MVP Jokic Tishio Celtics NBA

Muktasari:
- Hilo lilikuwa taji muhimu kwa Celtics ya ukanda wa Mashariki kulibeba kwani liliifanya timu hiyo kufikisha mataji 18 ya NBA na kuwa timu ya kwanza kushinda mataji mengi zaidi kihistoria, awali walikua wakilingana na Los Angeles Lakers ya Magharibi.
BOSTON Celtics ndio mabingwa wa ligi ya kikapu Marekani (NBA) msimu uliopita kufuatia kuibuka mshindi ndani ya mechi tano za fainali ya jumla dhidi ya Dallas Mavericks kutokea ukanda wa Magharibi.
Hilo lilikuwa taji muhimu kwa Celtics ya ukanda wa Mashariki kulibeba kwani liliifanya timu hiyo kufikisha mataji 18 ya NBA na kuwa timu ya kwanza kushinda mataji mengi zaidi kihistoria, awali walikua wakilingana na Los Angeles Lakers ya Magharibi.
Hata hivyo, kabla ya kwenda kulibeba taji hilo msimu uliopita, timu hiyo haikuwa na uhakika wa kulibeba hadi pale waliposhangaa timu ya Denver Nuggets ikitolewa kwenye nusu fainali (playoffs) ukanda wa Magharibi na timu ya Minnesota Timberwolves.
Ni kwa sababu Celtics inaihofia zaidi Nuggets ya MVP wa msimu uliopita, Nikola Jokic ambao pia ndio walibeba taji hilo msimu wa nyuma yake na hadi kuelekea msimu ujao, ndio timu ambayo Celtics inaamini ni tishio kwenye jitihada zao za kutetea taji hilo kama alivyoeleza staa wao namba moja Jayson Tatum.