Msiombe Arteta apate hii timu

Muktasari:
- Kwa misimu mitatu mfululizo, Arsenal imekomea kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England ikishindwa kubeba taji hilo. Sasa inataka kufanya usajili wa kibabe ili kubeba taji.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL bado haijakamilisha dili la maana kwenye dirisha hili, lakini kama wachezaji wake wote inaowataka ikiwanasa, basi chama la Mikel Arteta litakuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao.
Kwa misimu mitatu mfululizo, Arsenal imekomea kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England ikishindwa kubeba taji hilo. Sasa inataka kufanya usajili wa kibabe ili kubeba taji.
Msimu uliopita, ishu kubwa iliyoelezwa kuwagharimu ni kukosekana kwa Namba 9 wa maana kikosini.
Hilo ndilo linalowasukuma kwenye dirisha hili kuingia sokoni kunasa huduma ya straika wa kiwango cha dunia, ikiripotiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la Viktor Gyokeres.
Kabla ya uamuzi wa kumchukua Gyokeres, Arsenal ilimshindanisha na straika mwingine, Benjamin Sesko kuona ni nani atafaa zaidi kwenye kuongoza safu yao ya ushambuliaji.
Mastraika wote hao wawili ni balaa, lakini Arsenal inaamua kwenda na Gyokeres, ambaye alifunga zaidi ya mabao 50 akiwa na kikosi cha Sporting Lisbon msimu uliopita.
Kwenye eneo la kiungo, Arsenal ina watu wa maana akiwamo Declan Rice na Martin Odegaard kwenye dirisha hili itamwongeza Martin Zubimendi na kwa sababu imempoteza kiungo Thomas Partey, hivyo nafasi yake itachukuliwa na Christian Norgaard kuja kuziba pengo hilo.
Eneo la ushambuliaji lilionekana kuwa tatizo kubwa. Arsenal haina watu wenye uchu na hatari kwa kufunga mabao kama Mohamed Salah na Erling Haaland na ndiyo maana inahitaji saini ya Gyokeres.
Kocha Mikel Arteta amekuwa akihitaji winga wa kulia pia na kwenye hilo timu yake imekuwa ikihusishwa na mkali wa Real Madrid, Rodrygo ili kuja kusaidiana na Bukayo Saka kufanya safu ya ushambuliaji ya Arsenal kuwa kiwembe huku mshambuliaji wa kati, yeyote tu atakayekuwapo kama ni Sesko au Gyokeres hakuna kitakachokuwa kimeharibika, atakuwa bize kupachika mipira nyavuni.
Washambuliaji wengine kama Kai Havertz, Gabriel Jesus na Gabriel Martinelli pamoja na wengine akiwamo Leandro Trossard watalazimika kuanzia benchini endapo kama watakuwa hawajapigwa bei.
Kwenye safu ya ulinzi, ameongezwa kipa Kepa Arrizabalaga, huku mabeki mabeki wa kati kina William Saliba na Gabriel wakitarajia kubaki ili kutimiza ndoto za timu hiyo ya kubeba taji la Ligi Kuu England.
Kikosi cha ndoto: Raya; Timber, Saliba, Gabriel, Lewis-Skelly; Rice, Zubimendi; Saka, Odegaard, Rodrygo; Gyokeres.