Mastaa kibao wahudhuria maziko ya Jota

Muktasari:
- Virgil Van Dijk, Andy Robertson na kocha Arne Slot waliwasili sambamba na mastaa wa zamani wa Liverpool, Jordan Henderson na James Milner mapema tu asubuhi Jumamosi waliwasili Ureno.
LISBON, URENO: MASTAA wenzake Diogo Jota wa sasa na zamani kwenye kikosi cha Liverpool wamewasili huko Ureno kwenda kuhudhuria maziko ya mchezaji huyo aliyefariki dunia ajalini, Alhamisi alfajiri.
Virgil Van Dijk, Andy Robertson na kocha Arne Slot waliwasili sambamba na mastaa wa zamani wa Liverpool, Jordan Henderson na James Milner mapema tu asubuhi Jumamosi waliwasili Ureno.
Curtis Jones, Alexis Mac Allister, Conor Bradley, Federico Chiesa na Wataru Endo nao walikuwa miongoni mwa mastaa wa Anfield waliokwenda kuagana na kipenzi chao.

Maziko ya pamoja Jota, 28, na mdogo wake Andre Silva, 25, yalipangwa kufanyika kwenye kanisa la Igreja Matriz de Gondomar baada ya wawili hao wote kupoteza maisha kwenye ajali hiyo gari.
Dunia ya wapenda soka iliomboleza kifo cha mshambuliaji huyo, ambaye alipoteza maisha baada ya gari yake aina ya Lamborghini kupasuka tairi na kuwaka moto alfajiri ya Alhamisi.
Staa wa Manchester United, Diogo Dalot - ambaye mchezaji mwenzake Jota kwenye timu ya Ureno, alionekana kuhudhuria Capela da Ressureicao huko Gondomar, Ijumaa.
Nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, ambaye ni Mreno pia aliwasili msibani akiwa na mkewe.

Mrembo Rute Cardoso ambaye alifunga pingu za maisha na Jota siku 11 zilizopita, aliwasili huko Sao Cosme Chapel katika mji wa nyumbani wa Jota wa Gondomar uliopo karibu na Porto, kaskazini mwa Ureno, mapema Ijumaa kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Mrembo, Rute, 28 ni mama wa watoto watatu, ambaye alizaa na straika huyo, alisafiri na mwili wa mumewe, aliyefariki dunia Hispania akiwa na mdofo wake, ambaye pia ni mwanasoka, Andre Silva.
Mji wa Gondomar ulikuwa na waombolezaji mbalimbali tangu Alhamisi ilipotokea ajali hiyo. Jota na mdogo wake, Andre, walikuwa ndani ya gari yao ya kifahari, Lamborghini yenye thamani ya Pauni 210,000 wakati ilipopasuka tairi na kuwaka moto kwenye barabara ya A52 huko Zamora, kaskazini mwa Hispania.
Wawili hao walikuwa wakielekea kwenye bandari ya Santander kuwahi kivuko cha kuwapeleka Uingereza, huku staa huyo akitumia usafiri wa gari kutokana na kuzuiwa kupanda ndege baada ya kufanyiwa upasuaji wa mapafu.

Mama yake Jota, mrembo Isabel na babu yao walionekana wakiwa na huzuni kubwa kutokana na msiba huo. Mastaa kibao walituma salamu zao za pole, akiwamo staa wa Ureno, Pedro Neto, ambaye alionekana akiwa na jezi ya Chelsea iliyokuwa na majina ya Jota na Andre kabla ya The Blues kukipiga na Palmeiras kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani asubuhi ya kuamkia Jumamosi. Chelsea ilishinda 2-1 na kutinga nusu fainali.