Man United hii, itafanya jambo

Muktasari:
- Kocha Ruben Amorim amepanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake cha Old Trafford baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita. Man United ilimaliza msimu katika nafasi ya 15, huku kocha huyo Mreno akishindwa kutamba baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Mdachi Erik ten Hag.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeanza dirisha la usajili kwa kufungua pochi nene lakini huo ndio kwanza mwanzo, mambo bado hayajaisha.
Kocha Ruben Amorim amepanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake cha Old Trafford baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita. Man United ilimaliza msimu katika nafasi ya 15, huku kocha huyo Mreno akishindwa kutamba baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Mdachi Erik ten Hag.
Na mambo yalitibuka zaidi baada ya kuchapwa na Tottenham kwenye fainali ya Europa League.
Jambo hilo lilikuwa na athari mkubwa kwa klabu kwenye ishu ya uchumi, huku wengi wakiamini pesa inaweza kuwa tatizo katika kutimiza mipango yao ya usajili. Lakini, haipo tayari kuathiriwa na hilo.
Imeshatumia Pauni 62.5 milioni kunasa saini ya Mbrazili, Matheus Cunha kutoka Wolves. Hiyo ilikuwa nyongeza ya kwanza kwenye maboresho ya safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Amorim.
Cunha ni usajili wa mwanzo tu, huku Man United ikihitaji kuongeza wengine kadhaa, ambao watafanya miamba hiyo ya Old Trafford kuwa tofauti kabisa wakati inaanza msimu wa Ligi Kuu England kwa kumenyana na Arsenal katika mchezo wa kwanza.
Golini; Kipa Andre Onana ameshindwa kuonyesha ushawishi kwamba anastahili kubaki kwenye eneo hilo na Man United ipo tayari kumfungulia mlango wa kutokea, Monaco ikihitaji huduma yake. Na kwenye hilo, Man United inaweza kukimbilia kwa kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, ambaye mkataba wake umebaki mwaka mmoja tu huko Parc des Princes.
Beki; Man United iliwasajili Leny Yoro na Matthijs de Ligt kwa ajili ya eneo hilo na bado kuna wengine wanaweza kuja akiwamo kinda Diego Leon na beki staa wa Sporting Lisbon, Ousmane Diomande.
Eneo hilo lina mabeki wengi akiwamo Lisandro Martinez, Patrick Dorgu na Diogo Dalot. Diomande anatazamwa kama mtu wa kuja kumbadili Martinez, ambaye amekuwa akiumia mara kwa mara.
Kiungo; Kwenye eneo la kiungo, Man United ina watu. Manuel Ugarte ni mbadala mzuri wa Casemiro, wakati Bruno Fernandes ni mchezaji mwenye uhakika wa kuanza katika eneo hilo. Kuondoka kwa Christian Eriksen kunatoa nafasi kwa makinda wengine akiwamo Kobbie Mainoo kuwa na uhakika wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Fowadi; Safu ya ushambuliaji ni eneo ambalo Man United inahitaji kulifanyia maboresho makubwa. Mawinga Antony, Jadon Sancho na Marcus Rashford wote walitolewa kwa mkopo msimu uliopita na hawaonekani kuwa na maisha kwenye timu hiyo sambamba na Alejandro Garnacho na Rasmus Hojlund. Amad ni mchezaji pekee mwenye uhakika wa kupata nafasi kikosini. Cunha ameongezwa kwenye eneo hilo na bila shaka Bryan Mbeumo, naye atafuata huku straika Christopher Nkunku, akipigiwa hesabu za kuja kuongoza safu hiyo ya ushambuliaji, atakuwa akipishana na Joshua Zirkzee.
Kikosi kinachotarajiwa: Donnarumma; De Ligt, Maguire, Yoro; Mazraoui, Ugarte, Fernandes, Dorgu; Mbeumo, Nkunku, Cunha.