Mourihno, CR7 freshi barida!

ISTANBUL, UTURUKI: JOSE Mourinho ametoa kauli ya kikubwa juu ya supastaa Cristiano Ronaldo baada ya wawili hao kuripotiwa kuwa na uhusiano usiokuwa mzuri.

Ronaldo na Mourinho hawakuwa watu waliopatana sana licha ya kuwahi kuwa pamoja kwenye kikosi cha Real Madrid.

Tofauti zao ziliibuka baada ya Mourinho kutua Bernabeu mwaka 2010, muda mfupi akitoka kuipa Inter Milan ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa fainali iliyochezwa kwenye uwanja huo.  Wakati wakifurahia mafanikio yao wakiwa pamoja, wawili hao walikuwa hawaangaliani usoni, lakini Ronaldo hakuwa amependezwa na mbinu za kocha huyo.

Mourinho alikuwa akimkosoa Ronaldo kwa kitendo cha kuacha kukaba uwanjani, akitolea mfano kwenye mchezo wa fainali ya Copa del Rey dhidi ya Valencia, kitu ambacho kilimkasirisha sana supastaa huyo.

Wakala Jorge Mendes, ambaye ndiye anayewasimamia wawili hao, alijaribu kupambana kuweka uhusiano huo sawa, lakini haikuwa rahisi kiasi hicho.

Na uhusiano ulionekana kutibuka zaidi wakati Mourinho alipoondoka Madrid mwaka 2013, lakini mambo yanaonekana kubadilika kwa sasa.

Katika kuelekea mechi ya Old Trafford ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Man United ya Mourinho na Juventus ya Ronaldo mwaka 2018, kauli ya Special One ilionyesha ukomavu wa kocha huyo na namna asivyofuga chuki kwenye moyo wake.

“Ni moja ya wanasoka bora wa muda wote - ni hivyo tu,” alisema Mourinho akimzungumzia Ronaldo.

Kabla ya hapo, Ronaldo alisema kuhusu kufanya tena kazi na Mourinho, aliposema: “Kufanya kazi tena na Mourinho? Ndiyo, kwanini isiwezekane?”

Mourinho baadaye alisema bila ya kujali tofauti zake na Ronaldo, aliposema: “Kumnoa yeye ni nyakati za juu kabisa kwenye kazi yangu ya ukocha. Kocha na mchezaji wake wanaweza kuwa na tatizo, lakini hilo linaishia uwanjani.”