Mkakati maalum… Isak, Sesko kutua Arsenal

Muktasari:
- Arsenal haikufanya usajili wowote katika dirisha la majira ya baridi licha ya kuhusishwa na majina kadhaa yaliyokuwa sokoni, lakini jambo hilo lilikuwa ni kimkakati zaidi kwani kuna pesa nyingi imeandaliwa kwa ajili ya maboresho ya kikosi kwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
LONDON, ENGLAND: VIGOGO wa Arsenal wanaamini kuwa watavuna matokeo ya kutosajili mchezaji yeyote katika dirisha lililopita ifikapo mwisho wa msimu huu.
Arsenal haikufanya usajili wowote katika dirisha la majira ya baridi licha ya kuhusishwa na majina kadhaa yaliyokuwa sokoni, lakini jambo hilo lilikuwa ni kimkakati zaidi kwani kuna pesa nyingi imeandaliwa kwa ajili ya maboresho ya kikosi kwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kocha Mikel Arteta, ambaye aliweka wazi katika wiki za mwisho za dirisha la uhamisho lililopita kuwa timu hiyo inapambana kusajili wachezaji wapya kabla ya mambo kuharibika, ameweka mkwanja wa kutosha utakaosaidia kufanya maboresho makubwa zaidi yatakayoanzia na safu ya ushambuliaji.
Katika eneo hilo, Arteta ana majina ya mastraika wawili wa kwanza akiwa ni Alexander Isak na Benjamin Sesko.
Mpango wa kwanza wa Arteta ni kuona Isak kutoka Newcastle anasajiliwa na ikishindikana kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kinachohitajika na timu yake, wataangukia kwa fundi wa RB Leipzig, Sesko.
Newcastle wameripotiwa kuwa wanataka kumbakisha Isak kwa gharama yoyote na wanapanga kumuongeza mkataba wa mshambuliaji huyo.
Arsenal walifanya jaribio la kumchukua Sesko Juni mwaka jana lakini alikataa na kuamua kubaki Leipzig na kusaini mkataba mpya kabla ya Euro 2024.
Vilevile, Arsenal inataka kumsajili staa wa Athletic Bilbao, Nico Williams wakati Raheem Sterling akijiandaa kurudi Chelsea.
Mbali ya maeneo hayo, pia kutakuwa na mabadiliko makubwa katikati ya kiwanja msimu ujao, ambako Jorginho na fundi wa boli Thomas Partey wanatarajiwa kuondoka kama wachezaji huru baada ya kumalizika kwa mikataba yao.
Ikiwa wote wataondoka kama inavyotarajiwa, itahitajika kuwachukua wachezaji wengine.
Jorginho kwa sasa yuko katika mazungumzo na Flamengo ya Brazil anayodaiwa kusaini nayo mkataba wa awali na ilihitaji kumsajili mwezi uliopita lakini Arsenal ilikataa.
Katika kuhakikisha inaweka sawa eneo hilo, mikakati muhimu tayari imefanywa kuhusu uhamisho wa kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi ingawa Real Madrid inaweza kuingilia kati dili hilo.
Staa huyu ambaye anauzwa kwa Pauni 51 milioni, katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana alikataa kutua Liverpool licha ya ofa nono aliyowekewa.
Kipa namba moja wa Espanyol, Joan Garcia, naye yupo katika mipango ya Arteta kwa ajili ya kumpa ushindani David Raya na tayari mazungumzo na wakala wake yameshaanza.
Pia washika mitutu hawa wanahitaji saini ya staa wa Ajax, Jorrel Hato wakati huo huo wanatarajia kupitisha panga la kutosha kwa kuachana na Kieran Tierney, Jakub Kiwior na Oleksandr Zinchenko ambao si kipaumbele katika kikosi cha kocha Mikel Arteta.
Mbali ya wachezaji, mabosi wa Arsenal wapo katika mchakato wa kutafuta mkurugenzi wa michezo mpya atakayemrithi Edu na tayari kuna majina kadhaa nje ya Jason Ayto anayekaimu nafasi hiyo.
Kwa upande wa watu wa nje wanaoweza kuajiriwa katika eneo hilo ni Mkurugenzi wa Michezo wa Real Sociedad, Roberto Olabe na mchezaji wao wa zamani Tomas Rosicky, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Michezo wa Sparta Prague.