Mikosi yamuandama Pogba

TURIN, ITALIA. KIUNGO wa wa Juventus, Paul Pogba amesimamishwa kwa muda na Shirika la Kupima wanamichezo wanaotumia dawa za kuongeza nguvu michezoni (NADO) nchini Italia ikiwa ni baada ya kufeli vipimo.

Kwa mujibu wa gazeti la Corriere Della Serra, Pogba amefeli vipimo hivyo na anadaiwa kukutwa na ongezeko la homoni za testosterone ambapo ikiwa uchunguzi wa mwisho utaonyesha kuwa kweli alitumia madawa basi atafungiwa kujishughulisha na michezo kwa miaka minne.

Pogba ambaye alifanyiwa vipimo hivyo kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Italia ambapo hakucheza hadi sasa hajasema chochote juu ya kusimamishwa kwake huko.

Kupitia taarifa iliyotolewa na mahakama ya kitaita ya kupambana na dawa za kulevya kwa wanamichezo nchini Italia
ilieleza kwamba:

"Mahakama ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya inatangaza kwamba, kwa kukubali ombi lililopendekezwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kitaifa wa Kupambana na Dawa za Kulevya, imechukua hatua ya kumsimamisha mwanasoka  Paul Pogba kwa kukiuka  kifungu cha 2.1 na 2.2"
wa upande wao Juventus pia walitoa taarifa ya kuthibitisha kupokea taarifa hiyo baada ya vipimo vilivyofanyika Agosti 20, 2023.

Wakala wake Rafaela Pimenta alipohojiwa na Tuttosport kuhusiana na suala hili alisema: "Tunasubiria uchambuzi zaidi wa vipimo na taarifa kamili, kwa sasa hatuwezi kuzungumza chochote, lakini nina uhakika Pogba hajawahi kukiuka sheria na ninaweza kuhakikisha hilo."