Messi: Mbappe? Hatuna tatizo

PARIS, UFARANSA. SUPASTAA wa Paris-Saint Germain,  Lionel Messi ameweka wazi hana tatizo na mchezaji mwenzake Kylian Mbappe baada ya fainali ya Kombe la Dunia 2022 kumalizika ambapo Argentina iliichapa Ufaransa kwa mikwaju ya penalti.

Messi amesema baada ya mchezo huo wa fainali haikuhathiri uhusiano wake na Mbappe licha ya maneno mengi kuzungumzwa mtandaoni. Mbappe alifunga hat-trick kwenye fainali hiyo akiisawazishia timu yake, mpira ukaamuriwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya sare ya mabao 3-3.

Hata hivyo, Ufarana ikaangukia pua na kuvuliwa ubingwa na Argentina ambayo ilikuwa moto wa kuotea mbali kwenye fainali za huko Qatar.
Mashabiki wengi wakajiuliza baada ya fainali hiyo uhusiano wa Messi na Mbappe utatetereka kati yako lakini Messi akapinga kauli hizo.

"Ndio mimi na Mbappe tunaongea kuhusu fainali, nilimwambia jinsi watu wa Argentina walivyofurahi, nilimuelezea kila kitu mpaka sherehe za ubingwa, hakuna kingine zaidi ya hapo," alisema Messi

Aidha Messi hakutaka kuendelea kuzungumza mambo ya fainali ya Kombe la Dunia ambayo yameshapita kwasababu anaelewa maumivu aliyopata Mbappe baada ya kukosa ubingwa.

Messi alivumilia maumivu aliyopata baada ya kukosa ubingwa wa Kombe la Dunia 2014 walipocheza kwa Ujerumani, lakini sasa anafurahia mafanikio waliyopata Qatar na wachezaji wenzake.