Mbappe kupewa jezi ya Modric Madrid

Kylian Mbappe

Muktasari:

  • Mbappe atakwenda kurithi Namba 10 kutoka kwa kiungo Luka Modric, ambaye mkataba wake huko Real Madrid utafika ukomo mwishoni mwa msimu huu. 

Madrid, Hispania. Real Madrid imeriporiwa kumwandalia supastaa Kylian Mbappe jezi yenye Namba 10 mgongoni wakati atakapojiunga nayo kwenye majira yajayo ya kiangazi akitokea Paris Saint-Germain.

Mbappe atakwenda kurithi Namba 10 kutoka kwa kiungo Luka Modric, ambaye mkataba wake huko Real Madrid utafika ukomo mwishoni mwa msimu huu. 

Luka Modric

Modric mwenye umri wa miaka 38 amekuwa na wakati mgumu katika kupata namba msimu huu na kutokana na hilo bila shaka itakapofika mwisho wa msimu huu itakuwa mwisho kwake.

Mbappe amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Santiago Bernabeu kwa miaka michache ya karibuni, ikiwamo kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Fowadi huyo Mfaransa aliwekwa nje ya kikosi cha Paris Saint-Germain kwa muda baada ya kuiambia klabu hiyo kwamba hana mpango wa kuongeza mwaka zaidi wa kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho.

PSG ilifanya jaribio la kumuuza mshambuliaji huyo mwaka jana, lakini ilishindwa kabla ya kumruhusu kuitumikia tena timu hiyo ya kocha Luis Enrique na kiwango chake cha sasa ni moto balaa.

Wakati dili lake la sasa likitarajiwa kufika ukingoni Juni, Mbappe alimwambia rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi kwamba ataachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.

Ripoti zaidi zinadai kwamba rais wa Real Madrid, Florentino Perez ameshawaambia mastaa wa kikosi cha kwanza cha Los Blancos kwamba Mbappe atajiunga nao bure kwenye dirisha lijalo la usajili.

Wakati huo, Mbappe amekuwa ahihusishwa pia na klabu za Ligi Kuu England, lakini kinachoonekana mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ataondoka Paris kwenda Madrid kwa ajili ya msimu ujao.

Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, Real Madrid imejiandaa kumpa Mbappe jezi Namba 10 atakapokamilisha uhamisho wake wa kutua Santiago Bernabeu. Kwa sasa staa huyo huko PSG anavaa jezi Namba 7, ambayo kwenye kikosi cha Los Blancos inavaliwa na Vinicius Junior, na Mbrazili huyo hana mpango wa kuiachia.
Kwa msimu huu, Mbappe amefunga mabao 32 katika mechi 31 za kimashindano.