Mbappe akubali lawama Ufaransa

Muktasari:
- Mbappe ambaye amejiunga na Real Madrid dirisha hili akitokea PSG, amefunga bao moja tu tena kwa njia ya penalti katika mechi sita alizocheza akiwa na Ufaransa kwenye michuano hiyo.
PARIS, UFARANSA: BAADA ya taifa lake kutolewa na Hispania kwa kichapo cha mabao 2-1, katika michuano ya Euro, staa wa Ufaransa Kylian Mbappe amekiri hakuwa bora katika michuano hiyo ya mwaka huu.
Mbappe ambaye amejiunga na Real Madrid dirisha hili akitokea PSG, amefunga bao moja tu tena kwa njia ya penalti katika mechi sita alizocheza akiwa na Ufaransa kwenye michuano hiyo.
“Katika soka ni aidha umefanya vizuri au vibaya, kiukweli sikufanya vizuri na michuano ya Euro kwangu ilikuwa ni an-guko, nilihitaji kuwa bingwa wa michuano hii, lakini imeshindikana,” alisema Mbappe.
“Kwa sasa nitaenda mapumzikoni, najua baada ya hapo nitakuwa vizuri na nitakuwa tayari kuanza maisha mapya, bado nina vitu vingi vya kufanya.”
Staa huyu mwenye umri wa miaka 25, alikuwa msaada mkubwa kwa Ufaransa akiiwezesha kushinda Kombe la Dunia mwaka 2018.
Vilevile walifika fainali ya mwaka 2022 na kupoteza taji hilo mbele ya Argentina.
Mbappe amesema moja ya sababu zilizochangia asifanye vizuri katika michuano ya mwaka huu ilikuwa ni jeraha la pua alilopata.
“Ilichangia kufanya vibaya kwangu katika michuano hii, nilijaribu hadi kuongea na dokta kama naweza kucheza bila ya maski lakini ilikuwa ngumu mwanzoni.”