Mastaa Ulaya wapata tuhuma nzito Afrika

PARIS, UFARANSA. SIRI imefichuka. Soka la Afrika limekuwa likikumbwa na kashfa nyingi sana za madai ya imani za kishirikina na mataifa mengi yamediriki hata kutuma waganga kwenye mechi za timu za taifa au klabu ili kusaidia zipate ushindi.

Kwa Afrika inaonekana ni jambo la kawaida na timu zimekuwa zikizidiana ujanja nje ya uwanja. Pia wachezaji wamekuwa wakituhumiana kurogana au kufanyiana mambo ya kishirikina.

Sasa unaambiwa, huku barani Ulaya haya mambo nayo yapo na wachezaji wamekuwa wakifanya ili tu kujilinda au kuzisaidia timu zao. Mbali na wachezaji, timu pia zimekuwa zikifanya ili kupata ushindi.

Baadhi ya wachezaji waliotajwa ni wa Ufaransa na miongoni mwao ni Paul Pogba. Inadaiwa wachezaji hao wanapenda kwenda kwa waganga kwa ajili ya tiba mbalimbali za kisoka.

Kiungo huyo anayekipiga Juventus ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A, aliwahi kuhusishwa na kashfa ya ushirikina lakini alipinga madai hizo.

Inaelezwa kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa na mshindi wa Kombe la Dunia mwaka 2018, anapenda kwenda kwa waganga ili kupata kinga kwa ajili ya kujikinga anapokuwa dimbani na aliwahi pia kutuhumiwa na kaka yake alimroga nyota mwenzake wa Ufaransa, Kylian Mbappe.


WIVU WAHUSISHWA

Sheikh mmoja aliyefahamika kwa jina la Issa ambaye ni mganga wa jadi aliwahi kusema, “Kuna wivu mwingi kwenye soka,” alisema kauli hiyo huku akinyanyua kipande cha gome na chupa ya dawa ya rangi ya njano.

Hiyo inamaanisha wachezaji wengi wanapenda kwenda kwa waganga wenye asili ya Afrika huko Paris ili kutafuta njia ya kujiepusha na watu wabaya na mambo mengine ndani ya uwanja.

Tangu Pogba alivyotuhumiwa alimroga Mbappe, ishu za kichawi kwenye soka zimeanza kudhihirika, kwa mujibu wa ripoti.

Sheikh akaongeza; “Hii rangi ya njano mara nyingi naitumia kumtibu mchezaji asipate majeraha, Pia naitumia kwa mchezaji ambaye mara nyingi anaumia kwenye mechi kubwa. Ndiyo huwa naitumia kumtibu mchezaji ambaye anaendelea kuumia kwenye michezo mikubwa,” alisema Sheikh Issa ambaye hilo sio jina lake halisi.

Imeelezwa mganga huyo ambaye amezaliwa Ivory Coast ana uwezo wa kusafisha nyota na amesisitiza pia ana uwezo wa kuona mambo yaliyopita na yajayo.

Mchungaji Joel Thibault, ambaye ni mshauri mkuu wa mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa na AC Milan, Olivier Giroud alisema: “Wanamichezo huwafuata waganga wa kienyeji mara kwa mara kwa mambo ya kishirikina.”

Inaelezwa haya yamekuwa yakifanyika kwa siri kubwa na moja ya tukio lililovuta hisia ni lile la Pogba na kaka yake, Mathias ambaye pamoja na watu wake wa karibu walijaribu kumlaghai Pogba awape pesa lakini ilishindikana, ndio kaka huyo akafichua mdogo wake huyo (Pogba) alimlipa mganga ili amroge Mbappe. Hata hivyo, nyota huyo ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni pamoja na mganga huyo walikataa tuhuma hizo.

Mganga huyo alisema pesa ndefu aliyolipwa na Pogba ni kwa ajili ya kazi yake (mganga huyo) nzuri Afrika. Hata hivyo, baadhi ya watu walipinga kauli ya mganga huyo na kati yao walidai alilipwa kwa mambo ya kishirikina, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na AFP mwaka 2020, ambalo limekuwa likifuatilia matuko kama hayo.


MASHARTI KWA WACHEZAJI

Kwa mujibu wa AFP, wanasoka wamekuwa wakipishana kwa waganga na wengi wanaenda kwa ajili ya mambo binafsi ikiwamo kujilinda na kadhia za uwanjani kama kuumia na mambo mengine.


Gilles Yapi Yapo- (nyota wa zamani wa Ivory Coast) alisema,

“Ilikuwa kama mzunguko,” alisema Gilles Yapi Yapo, nyota wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast anayedai alitapeliwa Euro 200,000 na mchawi.

Kiungo huyo ambaye sasa anasimamia timu inayoshiriki ligi daraja la pili Uswizi, alikuwa akipitia kipindi kigumu wakati akiichezea Nantes ya Ligi Kuu ya Ufaransa maarufu Ligue 1, mjomba wake alipendekeza akamwone mganga wa jadi huko huko Paris.

“Sikuvutiwa sana na uchawi,” Yapi Yapo aliiambia AFP, ambaye alikulia Ivory Coast na jambo la kwenda kwa mganga ilikuwa kawaida.

Mganga huyo alisema familia yake “imelaaniwa”, jambo ambalo lilikuwa likimzuia kufanikiwa na kuwa na furaha na kumwamuru kutoa sadaka kama mbuzi, kondoo, na jogoo ili kukabiliana na laana”.


KUMTOA KAFARA MTOTO

Sadaka zilizohitajika ili kupata utajiri zinagharimu Pauni 40,000, 50,000, au 60,000”.

Hata hivyo, Yapi Yapo ameendeelea kusema alipokwama kiuchumi, mganga huyo alimuambia kama hana pesa itabidi amtoe kafara mtoto wake. “Nilishangaa sana, nilipata nguvu na kuondoka na sikurudi tena kwa mganga huyo.”

Alisema imani yake ya Kikristo ilimsaidia kumpa nguvu ya kujizuia kwenda kwa waganga, pia alisema baadhi ya waganga walitishia kulipa kisasi.


WANAKIMBILIA AFRIKA

Joel Thibault, mchungaji wa kiinjilisti wa mastaa kadhaa wa huko Ufaransa, akiwemo straika wa AC Milan, Giroud. amelazimika kukabiliana na “matokeo mabaya” ya wanasoka na wachezaji wa mpira wa vikapu walionaswa katika mazingira ya aina hiyo.

“Najua kuna klabu zinaruhusu wachezaji kwenda Senegal baada ya kupata majeraha kwa sababu madaktari hawawezi kuwatibu. Wanarudi na kucheza na hirizi na mikanda ya ulinzi,” Thibault aliongeza.


ISHU YA POGBA

Mchungaji Thibault alisema kesi ya Pogba baada ya nyota huyo wa Ufaransa kushikiliwa kinyume na matakwa yake mwaka jana, kwa ajili ya ulaghai wa unyang’anyi ilizua sintofahamu iliyohusu familia yake.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia wa Ufaransa alilaumiwa na kaka yake Mathias Pogba na rafiki yake wa utotoni kwa kumlipa mganga ili kumroga mchezaji mwenzake wa Ufaransa,  Mbappe, madai ambayo Pogba na mganga huyo walikanusha kwa polisi.

Anasema mchungaji huyo ambaye ni muinjilisti, “Wachezaji wananiambia kila wakati wanapotaka kufanya vipimo vya kuzuia matumizi ya dawa za kusisimua misuli, madaktari hawawezi kuwachoma sindano hadi wawapigie simu waganga wao ili kutoa ruhusa, hiyo inamaanisha jinsi gani ishu hii inafahamika na kila mtu,” Thibault alisisitiza.


WAGANGA WAFUNGUKA

Wakati huo huo, waganga kadhaa wameibuka na kusema kwa sasa wananyanyapaliwa kutokana na sakata la Pogba baada ya kugundulika amejihusisha na ushirikina.

Mganga mmoja kutoka Guinea, Monsieur Fakoly alisema aliwahi kufanya kazi nje ya Paris na amesisitiza watu wanatakiwa kutofautisha waganga wanaoroga na wanaosaidia watu.”

Sasa kwa mujibu wa AFP imegundua kwa nini waganga wanaogopwa na kunyanyapaliwa kwa mujibu wa mwanaanthropolojia na sababu ya waganga kutawala katika baadhi ya jamii.


ZAWADI ZAHUSISHWA

Sheikh Issa anavalia suruali ya ‘jeans’ mtaani, lakini anapowakaribisha wateja wake kwenye upasuaji wake huvaa vazi refu la ‘boubou’ la Kiafrika. “Siamini katika hirizi, naamini katika Quran na mimea,” alisema mganga huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye pia anafanya biashara ya kusafisha nyota.

Baadhi ya zana zake za biashara yake zinaonekana zimepangwa karibu na chupa kadhaa na mifuko ya plastiki - gome la mti ambalo hukukinga kutoka kwa “jicho baya”, mbegu za kusaga ambazo zinakuwezesha kukupa bahati na dawa za mafanikio kwa wanasiasa na wafanyabiashara.


NYOTA ZA WATU

Waganga wengi wa Afrika Magharibi wanaofanya upasuaji Ufaransa ambao wanajiona kama waganga wa roho wamejifunza kukabiliana na walaghai wa wateja wao wa Ufaransa.

Wengi huenda kwao kama watu wengine wanvyokwenda kwa mwanasaikolojia kama wanavyosema wataalamu.

Mwanaanthropolojia, Liliane Kuczynski, mwandishi wa kitabu cha uhakika ‘African marabouts in Paris’, alipata wateja wanaotoka katika wigo mpana wa kijamii, kutoka kwa wahamiaji wasio na vibali hadi wahitimu na walimu.

Lakini Monsieur Fakoly, mganga wa Guinea anayefanya kazi mjini Paris, ambaye anatoka kwenye safu ya marabouts, alikuwa na maoni yake kuhusu jinsi inavyofanya kazi. “Kila mmoja wetu ana nyota, ikiwa chafu inatakiwa kusafisha, watu wanashindwa na wana bahati mbaya,” alisema.


SHUHUDA AFUNGUKA

Raymond, 61, alikuwa amewasili katika chumba cha mashauriano cha Sheikh Issa huko Paris. Shekhe taratibu akampa mkono huku akibonyeza kidole gumba na kumwambia anahisi mambo si mazuri.”

Kisha Raymond akachukua kalamu na kuileta midomoni mwake bila kusema neno lolote. Katika ukimya huo, sheikh aliandika kwenye daftari lake, kisha akafuatilia baadhi ya mistari kati ya herufi ili kuibua “roho 16” kwa kutumia mbinu iitwayo geomancy. Kijana huyo alienda kwa mtaalamu huyo baada ya kugundua mke wake amemroga baada ya kufanyiwa matibabu baada ya wiki kadhaa hali ilirejea kama kawaida na akathibitisha alipompatia pesa mganga huyo.


WALAGHAI

“Baadhi ya waganga ni kama madaktari wa kisaikolojia huku wengine ni walaghai,” alisema mwanaanthropolojia, Jean-Pierre Olivier de Sardan wa Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Kisayansi cha Ufaransa (CNRS).

Alisema waganga wengine wana hatari ya kufosi watu badala ya kukabiliana na hali halisi, waganga wanawashawishi watu matatizo yao yamesababishwa na uchawi kutoka kwenye familia zao, ambayo inaweza kusababisha wasiwasi na huzuni na jitihada zinafanyika kuvunja miiko ya kichawi.

Lakini sera za Ufaransa hujihusisha na malalamiko kuhusu ulaghai au kutumia dawa kinyume cha sheria, aidha kesi kama hizo ni nadra na zinapigwa marufuku kuzungumzwa alisema Assa Djelou.


KUWATEGEMEA WAGANGA WA JADI

Katika michezo, ambapo ushirikina ni jambo la kawaida, mambo yanaweza pia kutokea kwa haraka.

Mchezaji akipata jeraha kidogo inaweza kuwa janga, alisema mchungaji Thibault kwa mara nyingine. mchungaji huyo kutoka Ufaransa amesisitiza, wakati mwingine wachezaji wanahitaji msaada kwa sababu hawana nguvu za ndani za kushinda kila kitu wakikabiliana na matatizo, lakini wanachofanya waganga ni hatari sana.”

Mchezaji wa zamani, wa Ivory Coast, Cisse Baratte aliiambia AFP, jinsi alivyoangukia chini ya ushawishi wa waganga kwa ajili ya kwenda Ufaransa kucheza soka na alitoa sadaka mbalimbali ili kufikia malengo yake.

Kocha maarufu huko Ufaransa, Claude Le Roy, ambaye alisimamia timu sita za taifa za Afrika, anafahamu mambo yote yanayohusu waganga wa jadi, kocha huyo alituhumiwa kuwa mchawi wa kizungu kwa kutumia waganga wa jadi.

Ingawa anasisitiza hana imani na masuala ya uchawi, Le Roy bado anasumbuliwa na kumbukumbu ya mambo yaliyotokea kwenye mechi za kufuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa na katika mchezo wa kwanza PSG ilifungwa mabao 3-0 na ilitakiwa kushinda mabao manne au zaidi kwenye mchezo wa mkondo wa pili.

Ndio kilichomshangaza kocha huyo kwani PSG ilishinda mabao 5-0 na kufuzu na hivyo kuhusishwa na mambo ya kishirikina ikidaiwa ilimpa mganga wa jadi Euro 500 ili awasaidie kupata ushindi huo.