Prime
Kwaheri Diogo Jota, kamwe hautatembea peke yako

MAISHA yana thamani gani? haijulikani. Diogo Jota ameondoka duniani kama upepo. Unaacha utajiri mkubwa, kipaji kikubwa, umri mdogo, umaarufu katika kila pembe ya dunia na kisha unaondoka ndani ya sekunde chache tu huku dunia nzima ikiangua kilio.
Bahati nzuri hajatembea peke yake. Wale vichaa wale wa Anfield wana msemo wao wa ‘You will never walk alone’. Wanamaanisha hautatembea peke yako. Jota ameondoka akiwa na wengi tukimsindikiza. Sahau kuhusu ushabiki wa timu.
Sahau kuhusu kila kitu. Baada kukata pumzi kwa ghafla akiwa na mdogo wake, Andre Silva, Jota ametembea na sisi wote hapa kumsindikiza kwa hisia kali kule alilokwenda ingawa hatukujui. Ametugusa sana.
Familia ya mpira imeungana. Kuanzia Istanbul, Anfield, Kagera, Buenos Aires, Melbourne, Washington na kwingineko katika kila pembe ya dunia. Mashabiki wa klabu nyingine pia walimpenda Jota. Kuanzia Manchester United, Arsenal, Liverpool, Tottenham Hotspur, Manchester City, Real Madrid, Barcelona, Inter Milan na kila timu ya mpira wa miguu.
Kwanini? Tulimfahamu na kumpenda. Ametuacha ghafla akiwa bado anaendelea kucheza soka katika umri wa miaka 28 tu. Ametuacha tukiwa tunaishi katika dunia ya mazoea. Kwamba msimu uliisha lakini atarudi tena kama wachezaji wengine na atacheza tena msimu ujao. Iwe Liverpool au kwingineko.

Ndiyo, alikuwa mchezaji maarufu anayecheza katika timu maarufu. Wameondoka wachezaji wengi mahiri, lakini wengi ni wa zamani. Hawakuwa wanaucheza mpira katika viwango vya juu wakati wanafariki dunia. Kina Diego Maradona na Pele walikuwa wachezaji maarufu kuliko Jota, lakini waliondoka wakati umri ukiwa mkubwa na asilimia moja tu ya watu waliobaki duniani ndio ambao waliwaona wanacheza.
Jota ameacha majonzi. Hakuna mkanganyiko wa mawazo nyuma yake. Uwanjani alikuwa mfungaji mzuri wa mabao. Lakini yeye ni wale wachezaji ambao wanapendwa hata na mashabiki wa timu nyingine. Kama ilivyo kwa Heung-Min Son au Bernardo Silva. Hawana shida na mtu.
Klabuni, ukisoma hisia za watu wengi waliokuwa karibu naye katika timu wanakuambia Jota alikuwa mtu poa ambaye alikuwa haaachi kutabasamu kwa kila kitu. Sifa ya kwamba alikuwa ni mtu poa sana inatajwa hata na kocha wake aliyempeleka Anfield, Jurgen Klopp.

Hapa ndipo hisia zinapokuwa kali zaidi. Ni mmoja kati yetu. Na majuzi tu ametoka kufanya kile ambacho mashabiki wa timu yake - Liverpool wangependa afanye uwanjani. Ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na timu yao. Ubingwa wa 20 huku yeye akiwa anavaa jezi namba 20 uwanjani.
Kule Ureno ametoka kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya. Ureno sio timu ambayo inatwaa mataji mengi ya kimataifa kama walivyo wakubwa wa Ulaya na kwa kufanya hivyo alikuwa amefanya kitu kikubwa na kina Ronaldo.
Nyumbani, Jota alikuwa ametoka kumuoa mpenzi wake wa muda mrefu ambaye pia ni mama wa watoto wake, Rute Cardoso ambaye ana watoto naye watatu. Ghafla kila kitu kinabakia kuwa historia.

Jota anatuachia kumbukumbu gani nyuma yake? Kwa pale Anfield anatukumbusha namna alivyokuwa mchezaji wa mwanzo mwanzo kuanza kuitengeneza Liverpool mpya kwa ajili ya kuuvunja utatu mtakatifu wa Sadio Mane, Mo Salah na Roberto Firmino.
Utatu ulikuwa unacheza mechi karibu zote kwa mafanikio makubwa wakati ule wanafukuzana na Manchester City. Klopp alipoamini kwamba muda wowote utatu wake utahitaji nguvu mpya ndipo alipoivamia Wolves na kutoa Pauni 41 milioni kumpata Jota.
Jota pia anatukumbusha maisha ya kijana mhangaikaji kutoka daraja la kawaida kabisa la maisha. Alizaliwa Porto akaonyesha kipaji chake kikubwa katika Klabu ya Pacos de Ferreira kisha Atletico Madrid wakamuona akiwa mdogo. Hata hivyo hakuuweza muziki wa kocha mzuiaji, Diego Simeone akajikuta akitolewa katika mikopo miwili. Kwanza ilikuwa Porto ya kwao Ureno, kisha akapelekwa kwa mkopo Wolves halafu akauzwa jumla hapohapo Wolves.

Kinachonifurahisha katika historia hii ni kwamba Wolves ilimrudisha katika timu kubwa, Liverpool. Kuna wachezaji ambao huwa wanazama kila kukicha na kule Atletico Madrid kungeweza kubaki historia tu. Lakini, Jota alichakarika katika mikopo yake miwili na kisha kuuzwa jumla Anfield ambako alipata kitu kikubwa kuliko katika timu kubwa ambayo ilimtoa kwao Ureno akiwa mdogo, Atletico.
Amefia katika jezi namba 20 ya Liverpool na kwa watu wa Anfield ni kitu kikubwa. Niliwahi kuandika hapa karibuni namna ambavyo kwa miaka mingi Liverpool walikuwa wanawinda kufikisha taji la 20 ili kuifikia Manchester United baada ya kuzubaa kwa miaka mingi wakiwa mbele kiasi cha kufikiwa kwa mataji ya Ligi Kuu England na Manchester United ambao kuna wakati walikuwa wameiacha mataji 18 kwa mataji saba.
Lakini, pia alikuwa ameipa taji la ubingwa wa Ulaya Liverpool. Haishangazi kuona Liverpool wameistaafisha jezi yake namba 20. Na baada ya yote haya Mungu amempa timu nzuri ya kufia - Liverpool. Nawaheshimu Liverpool kwa ‘uwendawazimu’ wao wa soka. Najua namna gani watamuimba Jota kwa kipindi chote cha maisha yetu. Majukwaa ya Anfield daima yatasimama kwake.

Kingine ambacho nitamkumbuka Jota ni namna ambavyo alikuwa anaifunga timu yangu Arsenal kama vile alikuwa ametukodi. Tangu akiwa Wolves kisha Liverpool. Katika mechi 16 alizocheza na Arsenal Jota ameifunga timu yangu mabao manane na kutoa asisti mbili.
Dunia itamkumbuka Jota. Itamkumbuka na mdogo wake, Andre Silva. Wametutoka ghafla. Wanatukumbusha namna gani maisha ni mafupi. Ni vile tu kwamba duniani wanasoka wanabeba asilimia chache mno ya wakati wa dunia hii, lakini vifo hivi hutokea kila mahali. Kinapotokea kifo kama hiki cha kijana staa mwenye umri wa miaka 28 anayecheza soka katika kiwango cha juu, inatukumbusha tumkumbuke Muumba.