Manchester United kutumia akili kubwa kwenye usajili

Muktasari:
- Dirisha la usajili linaendelea Ulaya na miamba ya soka inapambana kuwania nyota wapya wa kwenda kuongeza kwenye vikosi vyao msimu ujao 2025/26 pamoja na zinazoshiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu.
MANCHESTER, ENGLAND: NDIYO. Manchester United haina presha kwenye masuala ya usajili kuhusu pesa na inatarajia kutumia pesa za mauzo ya mastaa wake kushusha vyuma vipya klabuni hapo.
Dirisha la usajili linaendelea Ulaya na miamba ya soka inapambana kuwania nyota wapya wa kwenda kuongeza kwenye vikosi vyao msimu ujao 2025/26 pamoja na zinazoshiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu.
Sasa baada ya kuwa na msimu mbovu uliopita, Man United imeanza usajili wake na tayari imeshamleta Matheus Cunha huku ikipambana kutaka kushusha mashine kali zaidi dirisha hili.
Kwenye suala hilo, ndipo mabosi hawataki presha na kuumiza vichwa na wanasubiri pesa za mauzo ya nyota wake akiwamo Alejandro Garnacho anayetarajiwa kuuzwa na Al Nassr ya Saudi Arabia inatajwa iko tayari kutoa kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 20, hayuko katika mipango ya Kocha Ruben Amorim na awali aliambiwa anaweza kutafuta timu nyingine kwa msimu ujao ili kupisha nyota wapya.
Awali Man United ilikataa ofa ya Pauni 40 milioni kutoka Napoli kwa ajili ya winga huyo, Januari mwaka huu na inaamini itapokea ofa nzuri kutoka klabu za Saudi Arabia.
Man United ambayo hali yake kiuchumi haiko sawa inatarajia pia kumuuza nyota wake Jadon Sancho aliyekuwa akikipiga kwa mkopo Chelsea na anatakiwa na timu za Saudi Arabia, huku pia tayari mezani kuna ofa ya Inter Milan inayohitaji huduma ya Rasmus Hojlund kwa mkopo wa msimu mmoja, kabla ya kumnunua jumla kwa Pauni 80 milioni.
Baada ya usajili wa Cunha kwa Pauni 62 milioni, Man United inatakiwa iuze baadhi ya nyota wake ili isije ikakiuka sheria za matumizi ya fedha na ikifanikisha mchakato huo, inaweza kutumia pesa hizo kuinasa saini ya Viktor Gyokeres kutoka Sporting Lisbon na inaelezwa amekubali kujiunga nao. Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden anapatikana kwa Pauni 60 milioni.
Man United pia inahitaji huduma ya straika wa Brentford, Bryan Mbeumo ambaye imeshafanya naye makubaliano binafsi na sasa inapambana kufikia makubaliano ya ada ya uhamisho na timu yake licha ya ripoti kudai Tottenham imeingilia kati dili hilo.