Prime
Uamuzi wa kushtua Simba, Camara atajwa

Muktasari:
- FAGIO kubwa na la kushitua linaweza likapita kwa Wana fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba kama kamati yenye dhamana ya kusajili itaendelea kushikilia msimamo inaouamini kwaajili ya kuisuka timu mpya ya makombe.
FAGIO kubwa na la kushitua linaweza likapita kwa Wana fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba kama kamati yenye dhamana ya kusajili itaendelea kushikilia msimamo inaouamini kwaajili ya kuisuka timu mpya ya makombe.
Kutokana na mwenendo wa timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali msimu huu pamoja na majadiliano na benchi la ufundi huenda wakafanya baadhi ya maamuzi ya kiufundi ambayo huenda yakashtua mashabiki lakini wao wanaamini hakuna mafanikio bila kuamua.
Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imeingia sokoni kusaka kipa na ikipata mtu wa kazi anayeendana na vigezo vyao, huenda ikaachana na Moussa Camara mwenye clean sheet 17 za Ligi Kuu. Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba uamuzi wa kutaka kumuacha Camara umebeba vitu vingi nyuma ya pazia vya ndani na nje ya uwanja ambavyo vitabaki kuwa siri ya muajiri na muajiriwa.
Kipa huyo ambaye amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu akifuta ufalme wa Aishi Manula, Simba wanaamini bado wanaweza kupata mbadala wake nje ya Tanzania na akawapa ufanisi mkubwa zaidi kwenye Ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Pamoja na mambo mengi kufanywa siri lakini Mwanaspoti linajua kwamba baadhi ya viongozi wa Simba wanaamini kwamba walihitaji zaidi ubora langoni hata katika ukuta kwenye Fainali ya Shirikisho na Nusu fainali Kombe la FA.
“Kuna mambo mawili yatakayowaondoa baadhi ya wachezaji Simba kiwango cha chini na wengine vitu vya ndani ambavyo ngumu kuvielezea ambavyo vingozi wamevibaini havina afya kwa malengo makubwa ya klabu,” kilisema chanzo hicho.
“Ukiachana na Camara kuna Fondoh Che Malone, Fabrice Ngoma ambaye jezi yake namba sita kuna mchezaji ambaye tukifanisha kumsainisha ndiye atavaa jezi yake, Joshua Mutale (asisti mbili) kuna viongozi wanataka abakie na wengine aondoke licha ya kiwango chake kuanza kuwaka dakika za mwisho,” kiliongeza chanzo chetu na kusisitiza kuwa huenda Simba ikaingiza sura nyingi za kazi msimu ujao lengo likiwa ni Ligi ya Mabingwa.
Mbali na hilo, chanzo hicho kilisema uongozi unaangalia uwezekano wa kumuacha kipa kati ya Ally Salim au Hussein Abel endapo wakimpata mlinda mlango mwingine mzawa wakimuwinda mmoja kutoka timu moja ya Ligi Kuu mkoani.
“Simba itafanya mabadiliko makubwa ukiachana na wale ambao wanatakiwa na timu nyingine kama Mukwala (mabao 12, asisti, tatu) ambaye anatakiwa na Kaizer Chiefs na RS Berkane likifanikiwa hilo itakuwa sababu ya kumbakiza Leonel Ateba (mabao 12, asisti tatu), vinginevyo alikuwa anapigiwa hesabu za kuondoka,” kilisema chanzo hicho.
Wachezaji wengine ambao Mwanaspoti linajua huenda wakaachwa ni Hussein Kazi(mkataba unaisha) na Aishi Manula ambaye pia mkataba wake umemalizika na anatajwa kujiunga na Azam FC ya Chamazi, Dar es Salaam.