Prime
Waarabu wavamia kambi ya Simba, mchongo mzima upo hivi

Muktasari:
- Achana na Steven Mukwala ambaye hivi karibuni Mwanaspoti ilikuhabarisha kwamba Waarabu wa Morocco, RS Berkane wamevutiwa na uwezo wake na kuweka mezani dau la Dola 300,000 (Sh793 milioni) wakitaka kumsajili.
BAADA ya Simba kufanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na kupoteza mbele ya RS Berkane, kuna jambo linakwenda kutokea likimuhusu kiungo muhimu wa kikosi hicho ambaye anatakiwa na Waarabu.
Achana na Steven Mukwala ambaye hivi karibuni Mwanaspoti ilikuhabarisha kwamba Waarabu wa Morocco, RS Berkane wamevutiwa na uwezo wake na kuweka mezani dau la Dola 300,000 (Sh793 milioni) wakitaka kumsajili.
Ishu mpya ni kwamba mabosi wa klabu ya Hassania Agadir ya Morocco, wapo katika mazungumzo ya kuipata saini ya kiungo nyota wa Simba raia wa DR Congo, Fabrice Ngoma, huku taarifa zikielezwa mchezaji huyo huenda akajiunga na kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao.
Ngoma aliyejiunga na Simba Julai 14, 2023, akitokea Al Hilal ya Sudan huku mkataba wake ndani ya Msimbazi ukitarajiwa kufikia tamati Juni 30, 2025, jambo linalotoa nafasi ya kusepa kirahisi kikosini hapo.
Taarifa kutoka Morocco, zinaeleza viongozi wa Hassania Agadir, wako hatua nzuri za kuipata saini ya nyota huyo ambaye amekuwa muhimili mkubwa wa eneo la kiungo cha Simba akishirikiana vizuri na Yusuph Kagoma.
Kituo cha Radio Mars cha Morocco, kimefichua viongozi wa Hassania wako hatua za mwisho za kuipata saini ya kiungo huyo kwa ajili ya msimu ujao, huku maslahi binafsi sio kikwazo kwao na kuanzia muda wowote dili hilo linaweza likakamilika.
Mwanaspoti linatambua nyota huyo alitaka kuondoka dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu, ingawa ushawishi wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids ukambakisha ili kutengeneza kikosi bora na cha ushindani katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, Simba ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ngoma aliyecheza timu mbalimbali ikiwemo, AS Vita Club na Mk Etancheite za DR Congo, Al-Fahaheel ya Kuwait na FC Ifeanyi Ubah ya Nigeria, amekuwa nyota tegemeo katika kikosi hicho, ingawa kwa sasa kuna uwezekano wa kuondoka kikosini.
Ikiwa dili hilo litatiki, itakuwa ni mara nyingine tena kwa nyota huyo kucheza soka nchini Morocco, baada ya awali kuichezea Raja Casablanca akitokea AS Vita Club ya DR Congo kuanzia Julai 1, 2019, hadi alipoondoka Agosti 8, 2022.
Msimu wake wa kwanza akiwa Simba, Ngoma alifunga mabao matatu ya Ligi Kuu huku msimu huu hadi sasa amefunga mawili na kuiwezesha timu hiyo kufika fainali ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32.
Simba imefika fainali baada ya miaka 32, tangu mara ya mwisho ilipocheza Kombe la CAF 1993, michuano iliyounganishwa na Kombe la Washindi mwaka 2004 ikazaliwa Kombe la Shirikisho Afrika ambapo kikosi hicho kikakosa ubingwa mbele ya RS Berkane ya Morocco.
Kikosi hicho, kimekosa ubingwa wa Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 3-1, baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Morocco kuchapwa mabao 2-0, Mei 17, 2025, huku marudiano yaliyofanyika visiwani Zanzibar, ikatoka sare ya bao 1-1, Mei 25, 2025.