Prime
Klabu zaigeuka Yanga

Muktasari:
- Yanga iliyotangaza kugomea pambano la Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba lililopangwa Juni 15, iliibua jambo jipya ikitishia kutocheza fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida Blck Stars hadi itakapolipwa fedha za zawadi kwa misimu mitatu kutoka TFF.
SAKATA linaloendelea baina ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga kuhusiana na deni la fedha za zawadi za ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA), limechukua sura mpya.
Yanga iliyotangaza kugomea pambano la Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba lililopangwa Juni 15, iliibua jambo jipya ikitishia kutocheza fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida Blck Stars hadi itakapolipwa fedha za zawadi kwa misimu mitatu kutoka TFF.
Katika madai hayo, Yanga iliorodhesha zawadi mshindi wa msimu uliopita kuwa ni Sh200 milioni jambo lililoshtua mashabiki wengi wa soka kwa vile wanajua kiwango cha zawadi kwa bingwa ni Sh50 milioni tangu michuano hiyo iliporejeshwa 2015, jambo lililosisitizwa pia na TFF jana.
Ipo hivi. Jana Jumatano, Yanga iliitwa TFF kupeleka nyaraka juu ya deni inalotangaza kuidai kutokana na zawadi ya Kombe la Shirikisho baada ya Jumatatu, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe kusema haitacheza fainali iliyopangwa kupigwa Juni 28 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar hadi itakapolipwa.
Yanga ilitwaa ubingwa huo 2023/2024 kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 6-5 dhidi ya Azam, fainali iliyochezwa Juni 2, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kamwe alinukuliwa akisema: “Taarifa hii iwafikie ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF na wadhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho kuwa hatutacheza mchezo wa fainali ya Juni 28 hadi tutakapolipwa hela yetu ya ubingwa kwa msimu uliopita. Tumevumilia dharau hizi kutoka kwa mamlaka za soka kwa muda mrefu sana. Sasa imefika mwisho. Hii ya Zanzibar pia hatutacheza.”
Hata hivyo, baada ya majibizano ya pande hizo mbili juzi Jumanne, TFF iliiita Yanga kupeleka ushahidi wa deni hilo, kwa vile inachojua ni kwamba fedha za timu hiyo zilikuwa zikilipia ada ya vibali vya usajili wa wachezaji na makocha wa ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, jana pande hizo mbili zilishindwa kupata muafaka na kuchukua sura mpya kwa kubainika zawadi za michuano hiyo hazijawahi kubadilika kutoka Sh50 milioni hadi kuwa Sh 200 milioni kama ilivyobainisha Yanga, na baadhi ya klabu zimenukuliwa zikisema zimeshtushwa na hilo.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Yanga ilieleza TFF imekuwa ilishikilia fedha za ubingwa wa michuano hiyo kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024, jambo ambalo ni kinyume na taratibu. Katika orodha hiyo Yanga imeainisha msimu wa kwanza deni ni Sh50 milioni kama ilivyo wa pili, ila uliopita iliweka 200 milioni.
Hata hivyo, jana Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine aliyezungumza na wanahabari baada ya kutoka ofisi za TFF, alisema hawana cha kujadiliana zaidi ya kutaka fedha zao za ubingwa wa michuano hiyo.
‘Wewe umeona wapi hela ya zawadi ikakatwa kwenye madeni? Sisi kwa upande wa Yanga hatutaki kujadiliana jambo lolote kwa sasa zaidi ya kudai haki yetu ya msingi ambayo ni fedha za ubingwa tuliochukua,” alisema Mtine.
Alipoulizwa ilipotokea Sh200 milioni, Mtine alisema ni wazi walipoelezwa kwamba shindano la sasa bingwa wanapewa kiwango cha Sh 50 milioni.
Akizungumzia kilichotokea jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo alisema Yanga haikutaka kuzungumza chochote katika kikao ilichoitiwa zaidi ya kuwasilisha barua kisha kuondoka.
“Baada ya Yanga kufika hawakutaka kuzungumza chochote zaidi ya kuleta barua ya kimaandishi kama waliyoitoa katika taarifa zao kwa umma,” alisema.
Ndimbo aliongeza hata Mtine alipotakiwa kuzungumza na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kuhusiana na sakata hilo hakuwa tayari.
“Kidao alitaka kuzungumza nao, lakini baada ya kuingia waliweka barua yao na kuondoka, kwani hawakutaka kuzungumza jambo lolote,” alisema Ndimbo na kufafanua kwamba zawadi ya bingwa wa Kombe la FA ni Sh50 milioni na si 200 milioni kama inavyodai Yanga. “Wakati mdhamini mpya wa michuano hii anaingia makubaliano na TFF, kila kitu kilikuwa wazi kwa sababu ilikuwa inajulikana fedha zile ni za uendeshaji, nasi ndio tunaopanga tuzitumie kwa namna gani, hivyo hakuna sehemu tuliyotangaza kama kiasi hicho kimeongezeka,” alisema Ndimbo.
KLABU ZAIGEUKA
Wakati Yanga ikishikilia msimamo wa kutaka kulipwa fedha za zawadi ikiorodhesha Sh200 milioni, baadhi ya klabu zimeigeuka zikidai haijawahi kutangazwa juu ya badiliko la zawadi za ubingwa wa michuano hiyo inayotoa mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabiti Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema klabu yao iliyocheza fainali mbili mfululizo zilizopita inachokijua ni kwamba zawadi za bingwa wa FA ni Sh50 milioni tangu michuano ikiwa chini ya udhamini wa Azam.
Zakazi aliongeza, hata wadhamini wapya walipoingia haikuwahi kuainishwa na TFF juu ya zawadi halisi ya michuano hiyo, zaidi ya shirikisho hilo kupanga lenyewe, hivyo wameshtushwa kusikia zawadi imeongezeka hadi Sh200 milioni.
“Hata hivyo, lakini hili lililoibuliwa linapaswa kutuamsha klabu nyingine kuanza kuulizia juu ya zawadi halisi za washindi na mambo yawekwe hadharani kwani ni fursa kwa klabu kujua kwa sababu tangu michuano iliporejea ikiwa kama ASFC zawadi ilikuwa ni Sh50 milioni tu,” alisema.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars iliyotinga fainali za msimu huu, Hussein Massanza alisema hawajapata mabadiliko yoyote juu ya ulipwaji wa fedha za bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho na sasa wapo katika mchakato wa kufuatilia kabla ya kuvaana na Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Massanza alisema wanachofahamu bingwa wa michuano hiyo analipwa Sh50 milioni, lakini sasa wameshtuka na kuanza kufuatilia kujua kama kuna mabadiliko baada ya kutinga fainali.
“Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ameanza mchakato wa kufuatilia endapo tutatwaa ubingwa tutapata kiasi gani kwa sasa, lakini miaka yote tunafahamu ni Sh50 milioni hatuna mabadiliko yoyote tuliyoyapata.”
Massanza alisema kuhusu mabadiliko inatakiwa kuzungumza na shirikisho ambalo ndilo linalosimamia masuala hayo na kwamba kitu pekee kinachotoka moja kwa moja ni zawadi ya mchezaji bora ambayo alithibitisha kuwa mchezaji wa kikosi hicho, Emmanuel Keyekeh baada ya kuibuka mchezaji bora wa mchezo alipewa moja kwa moja kutoka kwa wadhamini akitumiwa kwenye akaunti yake.
Mtendaji Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema hawana mabadiliko yoyote kuhusiana na fedha anayopokea bingwa wa mashindano.
“Tulicheza hatua ya fainali kiasi kinachotambulika miaka yote ndio tulichokuwa tunakifahamu. Kwa sasa sijui bingwa anachukua bei gani kama kuna mabadiliko sisi hatuna taarifa hiyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa utaratibu wa michuano hiyo kila hatua inayoshiriki timu kuna fedha inapewa kwa ajili ya mechi husika, japo kwa zawadi halisi ya bingwa haijawahi kujulikana tangu mdhamini mpya aiingie.
UDHAMINI ULIVYO
Michuano ya shirikisho ilirejeshwa 2015-2016 baada ya kusimama tangu 2002 na Azam Media ndio iliyokuwa ikiidhamini na bingwa ilikuwa ikipewa Sh50 milioni, kabla ya mwaka jana ilipoingia Benki ya CRDB kwa mkataba wa miaka mitatu.
Wakati ikiingia kuidhamini michuano hiyo benki hiyo ilianza kwa kutoa Sh255 milioni ikiwa hatua ya robo fainali na msimu huu ukiwa ni mwaka wa kwanza dau ni Sh800 milioni ambazo zinajumuisha maandalizi ya mashindano, zawadi ya bingwa na washindi wengine kama mchezaji bora wa msimu, nyota wa mchezo, bao bora na kadhalika.
Kwa msimu wa pili wa udhamini huo, dau litaongezeka kuwa Sh1 bilioni na msimu wa tatu ambao ndio wa mwisho wa mkataba itakuwa ni Sh1.2 bilioni.