Prime
Sura mbili mpya zaonekana mazoezini Simba

Muktasari:
- Achana na kiungo mzawa Morice Abraham (22) ambaye alikuwa na kikosi hicho akifanya mazoezi tangu Aprili mwaka huu, kuna nyota wengine wapya wawili.
KATIKA mazoezi ya Simba ambayo timu hiyo inaendelea kujiandaa na michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara iliyosalia, kuna sura mbili za wachezaji wapya wakijifua.
Achana na kiungo mzawa Morice Abraham (22) ambaye alikuwa na kikosi hicho akifanya mazoezi tangu Aprili mwaka huu, kuna nyota wengine wapya wawili.
Abraham ambaye alikuwa akiitumikia FK Spartak Subotica ya Serbia, kwa sasa ni mchezaji huru hivyo ametua mazoezini Simba kujiweka fiti kuelekea msimu ujao.
Simba imeanza kuwatesti mazoezini wachezaji wengine wawili wazawa mbali na Abraham ili kuwasoma kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuwasajili kwa msimu ujao.
Wachezaji hao wote ni washambuliaji ambapo Omary Marungu (22) kutoka Mtibwa Sugar na Crispin Kipenye aliyecheza Songea United katika Ligi ya Championship msimu uliomalizika hivi karibuni. Kipenye pia aliwahi kuitumikia timu ya vijana ya Simba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, wachezaji hao wapo ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kufanya majaribio na endapo wakilishawishi benchi la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids, huenda wakasajiliwa.
Kipenye msimu huu katika Ligi ya Championship akiwa Songea United, amefunga mabao manne na asisti saba, wakati Marungu akiisaidia Mtibwa Sugar kurejea Ligi Kuu Bara.
Marungu aliyewahi kucheza Hapoel Kfar Saba inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Israel, inaelezwa uwezo alionao umemridhisha kocha Fadlu na anaendelea kumtazama kwa ukaribu zaidi kabla ya kufanya uamuzi kama ilivyo kwa Morice ambaye alikuwa wa kwanza kutua hapo.
"Ni kweli kuna wachezaji hao wanafanya mazoezi na timu, wana nidhamu kubwa, hatma yao ipo chini ya kocha mkuu kama watafanya vizuri na kumridhisha kwa viwango vyao basi watasajiliwa na kuitumikia timu yetu," amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
"Umri wao na nafasi wanazocheza unashawishi kwani timu inahitaji nyota wa damu changa ili kusongesha gurudumu la timu yetu, tunaamini kama wataweza kufanya vizuri kwa nafasi hii waliyoipata tutakuwa na wachezaji wazuri ambao tayari wamezoea mazingira."
Chanzo hicho kilisema hadi sasa kocha Fadlu ameonyesha kufurahishwa zaidi na uwezo wa Marungu ambaye amemtaja kuwa ni mchezaji anayecheza vizuri kwa nafasi, ana kasi na nguvu akiamini kama ataendelea hivyo ataisaidia Simba.