Man U, Arsenal zapangiwa vigogo Europa

Friday February 26 2021
europa pic
By Mwandishi Wetu

Droo ya hatua ya 16 ya mashindano ya Ligi ya Europa imezipa kibarua kizito Manchester United na Arsenal baada ya timu hizo mbili kubwa England kupangwa kuumana na vigogo vya soka barani Ulaya AC Milan na Olympiacos katika hatua hiyo.

United waliotinga hatua hiyo baada ya kuitoa Real Sociedad kwa ushidi wa jumla wa mabao 4-0 wamepangwa kukutana na AC Milan ya Italia ambayo yenyewe imefuzu baada ya kuitupa nje timu ya FK Crvena Zvezda kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 kwenye mechi mbili baina yao.

AC Milan imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya United kwani katika nyakati tatu tofauti walizokutana kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Ulaya ambapo mara zote hizo ilisonga mbele ambapo ilikuwa ni katika misimu ya FK Crvena 1957/58, 1968/69 na 2006/07.

Lakini mechi hiyo itamkutanisha nyota wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic na Manchester United aliyowahi kuitumikia kwa misimu miwili kati ya mwaka 2016 hadi 2018 akiifungia mabao 29 katika mechi 53 na kati ya hayo, matano aliyafungwa katika mechi 11 za mashindano ya Europa msimu wa 2016/2017 ambao Manchester United walitwaa ubingwa.

Wakati United wakipangwa dhidi ya AC milan ambapo wataanzia nyumbani, Arsenal yenyewe itaanzia ugenini dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki.

europa pic 2
Advertisement

Timu hizo zimewahi kukutana mara nne katika mashindano ya Ulaya ambapo kila moja imeibuka na ushindi mara mbili ingawa Arsenal wanaingia wakiwa na kumbukumbu mbaya mbele ya Olypiacos kwani ndio iliwatoa kwenye mashindano hayo msimu uliopita baada ya kuwafunga mabao 2-1 nyumbani ingawa Arsenal alishinda bao 1-0 ugenini.

Ukiondoa timu hizo, Tottenham Hotspur imepangwa kucheza na Dinamo Zagreb, Ajax wataikabili Young Boys, AS Roma watacheza na Shakhtar Donetsk wakati Dynamo Kyiv wataikabili Villareal.

Mechi nyingine zitakuwa ni baina ya Slavia Praha na Rangers huku Granada ikikabiliana na Molde

Ratiba ya 16 Bora

Ajax vs Young Boys
Dynamo Kyiv vs Villareal
Manchester United vs AC Milan
AS Roma vs Shakhtar Donetsk
Olympiacos vs Arsenal
Slavia Praha vs Rangers
Dinamo Zagreb vs Tottenham
Granada vs Molde

Advertisement