Mabingwa Ulaya... Ni Man City, Real Madrid tena

Muktasari:
- Man City ya Pep Guardiola itakabiliana na Real Madrid katika mechi mbili za nyumbani na ugenini kati ya Februari 11 au 12 na Februari 18 au 19 baada ya timu zote mbili kumaliza hatua ya League Phase nje ya timu nane za juu ambazo zimefuzu moja kwa moja kutinga 16 bora.
LONDON, ENGLAND: USIYEMPENDA kaja. Unaweza kusema hivyo baada ya Manchester City kupangwa kumenyana na Real Madrid kwenye mechi ya mchujo ya kuwania tiketi ya kutinga mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya iliyopangwa leo Ijumaa.
Man City ya Pep Guardiola itakabiliana na Real Madrid katika mechi mbili za nyumbani na ugenini kati ya Februari 11 au 12 na Februari 18 au 19 baada ya timu zote mbili kumaliza hatua ya League Phase nje ya timu nane za juu ambazo zimefuzu moja kwa moja kutinga 16 bora.
Kwa nafasi iliyokuwa imemaliza Man City kwenye msimamo wa ligi hiyo, ilikuwa na ufahamu itakwenda kumenyana ama na Real Madrid au Bayern Munich kwenye hatua hiyo ya mchujo, lakini sasa imeshafahamu mpinzani wao, huku Wajerumani hao Bayern watakuwa na kibarua cha kuikabili Celtic ya Scotland.
Kwenye mechi nyingine za mchujo, Club Brugge itakipiga na Atalanta, Sporting Lisbon itamalizana na Borussia Dortmund, wakati Juventus itakuwa na mechi ya kibabe dhidi ya PSV Eindhoven huku Feyenoord ikionyeshana ubabe na AC Milan, Brest na Paris Saint-Germain na Monaco itamalizana na Benfica.
Baada ya kumaliza nafasi nane za juu kwenye league phase, Liverpool, Arsenal na Aston Villa zenyewe zimevuka moja kwa moja kutinga hatua ya 16 bora na hazitacheza kwenye mchujo kama ilivyo kwa Barcelona, Inter Milan, Atletico Madrid, Bayer Leverkusen na Lille.
Kwa timu za Ligi Kuu England zilizofuzu hatua ya 16 bora, Liverpool kwenye njia yao kuna mechi za Brest kucheza na PSG na Monaco kukipiga na Benfica, wakati kwenye njia ya Arsenal kuna mechi za Feyenoord na AC Milan wakati PSV Eindhoven itakipiga na Juventus, huku kule kwenye njia ya Aston Villa kuna mechi za Club Brugge na Atalanta na Sporting Lisbon itakipiga na Borussia Dortmund.
Mara tu mechi hizo za hatua ya mchujo zitakakamilika kutakuwa na droo nyingine ya kupata timu zitakazochuana kwenye hatua ya 16 bora. Kwa timu za Liverpool na Barcelona ambazo zimefanya vizuri kwenye raundi ya league phase, timu hizo hazitakutana kwenye hatua hiyo ya 16 bora.
Kwa Man City na Real Madrid baada ya kupangwa kumenyana tena hiyo itakuwa mara ya nne katika misimu mitano ya mwisho. Msimu uliopita, Man City ilisukumwa nje ya michuano hiyo kwenye hatua ya robo fainali na Real Madrid kwa mikwaju ya penalti, lakini vijana wa Pep Guardiola walishinda kwa jumla ya mabao 5-1 kwenye mechi ya nusu fainali dhidi ya Los Blancos, wakati walipokwenda kushinda taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023.
Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo imechezwa kwa mfumo mpya msimu huu, timu 12 zimeshaaga baada ya kukamilika kwa hatua ya makundi, wakati timu nane za juu zimetinga kwenye mtoano wa 16 bora.
Timu zilizoshika nafasi ya kuanzia namba 9 hadi 24, zitacheza mechi mbili za mchujo mwezi huu na kundi hilo linashuhudia timu zilizocheza fainali msimu uliopita, Real Madrid na Borussia Dortmund pamoja na mabingwa wa mwaka 2023, Man City.
Baada ya kushika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa league phase, nafasi moja nyuma ya Celtic, timu hizo mbili za Uingereza zilifahamu mapema zitachuana na timu zilizomaliza nafasi ya 11 na 12 kwenye mechi za mchujo ambazo ni mabingwa mara 15, Real Madrid na mabingwa mara sita Bayern Munich.
Droo ya hatua ya 16 bora itapangwa, Ijumaa ya Februari 21 baada ya mechi za mchujo kumalizika.
DROO KAMILI YA MECHI ZA MCHUJO LIGI YA MABINGWA ULAYA 2024-25
Club Brugge vs Atalanta
Sporting Lisbon vs B.Dortmund
Man City vs Real Madrid
Celtic vs Bayern Munich
Juventus vs PSV Eindhoven
Feyenoord vs AC Milan
Brest vs PSG
Monaco vs Benfica.