Lukaku awapa raha Chelsea

Wednesday September 15 2021
lukaku pic

CHELSEA imeanza harakati  za kulitetea  taji lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Romelu Lukaku dhidi ya Zenit St Petersburg.

Lukaku, ambaye alisajiliwa kwa Pauni 97.5milion akitokea Inter Milan, ameonekana kuwa mwarobaini wa kocha Thomas Tuchel kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Katika mchezo huo ambao vijana  wa Tuchel walikuwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Stamford Bridge, iliwabidi kusubiri hadi  dakika 69 kupata bao lililofungwa kwa kichwa  na Lukaku na yote hiyo ilitokana na upinzani ambao Zenit St Petersburg ilikuwa ikiuonyesha.

Haukuwa mchezo mwepesi kwa Chelsea kwani Zenit walionekana kuwa na mbinu madhubuti ambazo ziliwanyima uhuru matajiri hao wa London ambacho licha ya kumiliki mchezo huo kwa kiwango kikubwa lakini hawakuonekana kuwa na madhara.

Zenit  walionekana kuziba mianya ya mashambulizi kwa Chelsea huku wakijenga mashambulizi yao  kwa kustukiza hilo lilionekana kufanya kazi kwao kutokana na kikosi chao kuundwa na wachezaji wenye kasi hivyo ilikuwa  rahisi kwao kutekeleza mipango yao.

Hata hivyo uzoefu wa wababe hao wa London na ubora wa kikosi chao uliwabeba na kupata bao hilo ambalo lilikuwa la nne kwa Lukaku kwenye mashindano yote  tangu ajiunge na klabu hiyo huku likiwala kwanza kwenye ligi hiyo ya mabingwa Ulaya.

Advertisement

Karata ya pili kwa Chelsea kwenye hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakuwa, Septemba  29 huko Italia  dhidi ya Juventus ambao kwenye mchezo  wa kwanza    waliitandika Malmo dozi ya mabao 3-0.
Advertisement