Luc Eymael amtabiria makubwa Samatta

Tuesday September 28 2021
eymael pic

KOCHA wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ambaye kwa sasa yupo kwao Ubelgiji, anaamini nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini humo anaweza kurejea kwenye makali yake kutokana na mwanzo mzuri alioanza nao msimu huu wa 2021/22 akiwa na Royal Antwerp.

Ndani ya michezo minne aliyoichezea Royal Antwerp aliyojiunga nayo kwa mkopo akitokea Fenerbahce ya Uturuki, Samatta ameifungia timu hiyo bao moja na kutoa asisti moja kwenye mashindano yote, bao alilofunga ilikuwa upande wa Europa Ligi.

Eymael alisema Samatta ni mshambuliaji mzuri na kwa kiasi kikubwa inaonekana presha aliyokumbana nayo England ilimuondoa kwenye mstari lakini anaweza kusimama tena na kuonyesha makali yake kama ilivyokuwa msimu kadhaa iliyopita.

“Kwangu ni mchezaji mzuri na mwenye ubora wa aina yake kwenye kumalizia, nadhani ni kati ya washambuliaji wazuri kutoka Afrika, najua kwamba miezi michache iliyopita ilikuwa migumu kwake lakini naamini kuwa ni mchezaji mwenye ukomavu ndani yake.

“Ameanza vizuri msimu huu hivyo hilo linaweza kuendelea kujenga hali yake ya kujiamini na uzuri ni kwamba hii ligi sio ngeni kwake, anaweza kufanya vizuri na kuiteka tena Ulaya,” alisema kocha huyo ambaye baada ya kuondoka Yanga alijiunga na Stade Tunisien ya Tunisia.

Samatta ametolewa kwa mkopo na Fenerbahce wenye kipengele cha kusajiliwa moja kwa moja kutokana na kushindwa kuonyesha makali yake akiwa na miamba hiyo ya soka la Uturuki tangu ajiunge nayo akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu England ambako nako alichemka.

Advertisement

Nahodha huyo wa Taifa Stars, alikuwa gumzo Ulaya msimu wa 2018/19 ambao alifunga mabao 32 na kutoa asisti sita kwenye michezo 51 aliyoichezea KRC Genk ambayo ilikuwa klabu yake ya kwanza barani humo ambako alitua akitokea TP Mazembe ya DR Congo.

Akiwa Genk kiujumla Samatta alihusika katika mabao 96 katika mechi 191 akifunga 76 na asisti 20.

Advertisement