De Bruyne kujengewa sanamu

Muktasari:
- De Bruyne alicheza mechi yake ya mwisho katika Uwanja wa Etihad, City ikiifunga Bournemouth 3-1. Alicheza kwa dakika 70 kabla ya kutolewa, akihitimisha kipindi cha miaka 10 alichodumu Jiji la Manchester.
MANCHESTER, ENGLAND: KEVIN De Bruyne ameagana rasmi na mashabiki wa Manchester City usiku wa Jumanne, huku Kocha Pep Guardiola akitokwa na machozi baada ya kuthibitishwa sanamu ya heshima itajengwa kwa ajili ya nyota huyo wa Ubelgiji.
De Bruyne alicheza mechi yake ya mwisho katika Uwanja wa Etihad, City ikiifunga Bournemouth 3-1. Alicheza kwa dakika 70 kabla ya kutolewa, akihitimisha kipindi cha miaka 10 alichodumu Jiji la Manchester.
Wakati anafanyiwa mabadiliko na kuingia Nico Gonzalez, alionyeshwa heshima kubwa na mashabiki na uwanja mzima ulisimama na kuimba jina la De Bruyne, japokuwa alikosa nafasi ya wazi kipindi cha kwanza kufunga bao ambalo lingeweza kuwa na maana kubwa sana.
Baada ya mchezo huo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 33, alitembea uwanjani akiwa na familia yake yenye watoto watatu, huku mashabiki wakibaki kushuhudia tukio hilo la kihistoria huku uwanjani hapo zikionyeshwa video za watu mbalimbali waliowahi kufanya kazi naye wakimpa heshima, jambo lililomgusa Guardiola kiasi cha kumliza.
De Bruyne alisema: “Manchester ni nyumbani, hapa ndipo watoto wangu walipozaliwa. Nilikuja hapa na mke wangu nikiwa na nia ya kukaa muda mrefu, sikutegemea ingekuwa miaka 10, wala kufanya tulichokifanya kama klabu. Tumeshinda kila kitu, tumeikuza klabu hii na sasa kizazi kingine kitaendeleza.
“Nilitaka kucheza kwa ubunifu mkubwa na shauku, nilitaka kufurahia soka na natumai kila mtu alifurahia pia. Watu wote ndani na nje ya klabu waliniboresha zaidi ya nilivyokuwa. Imekuwa heshima kubwa kucheza na wachezaji hawa. Nimepata marafiki wa maisha, hakika nitarejea.”
Kiungo huyo aliendelea kusema: “Unataka kufanya vizuri na kushinda na ukishinda unataka kushinda zaidi. Tumekuwa na maandamano sita ya kusherehekea ubingwa ambayo hayatasahaulika, kushuhudia kila tukio na nyakati na wachezaji wenzangu limekuwa jambo la furaha isiyoelezeka.”
Akizungumzia kuhusu mashabiki wa City, alisema: “Wamekuwa wakarimu sana tangu mwanzo, lakini kuwa na uwanja mzima ukiunga mkono familia yangu na mimi ni jambo la kipekee. Nani mwingine anaweza kupata watu 50,000 wakisubiri kukuaga, hali hii haiwezi kuelezewa. Asanteni sana.”
Kuhusu kujengewa sanamu, alisema: “Inamaanisha nitaendelea kuwa sehemu ya klabu hii milele, nitawakilisha kipande kidogo cha historia. Kila nitakaporejea, nitaweza kuliona sanamu langu na kujua kuwa nipo hapa daima.”
Aprili mwaka huu, taarifa za De Bruyne kuondoka Man City zilithibitishwa baada ya hapo awali kuwepo tetesi, huku mkataba wake ukiwa unakaribia kumalizika. Alijiunga na Manchester City mwaka 2015 kutoka Wolfsburg kwa ada ya rekodi ya wakati huo, na tangu hapo amekuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Mbelgiji huyo ametwaa mataji sita ya Ligi Kuu ya England akiwa na City, pamoja na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023. Mchango wake binafsi umemletea tuzo nyingi, ikiwa ni pamoja na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa PFA mara mbili mfululizo.
Kinachofuata kwa sasa ni wapi De Bruyne anaelekea huku mwenyewe akiwa hajaweka wazi hilo kama atasalia barani Ulaya au hata kuendelea kucheza Premier League. Ingawa awali alihusishwa kuhamia Ligi Kuu ya Marekani, huku akisisitiza bado anataka kuendelea kucheza katika kiwango cha juu zaidi.