Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lamine kupewa jezi ya Messi

Muktasari:

  • Jezi hiyo ina heshima kubwa ndani ya Barcelona na mara ya mwisho Lionel Messi aliivaa kabla ya kukabidhiwa Ansu Fati ambaye ameonekana kushindwa kuitendea haki.

BARCELONA, HISPANIA: Barcelona inaripotiwa kufanya uamuzi wa kumpa Lamine Yamal jezi ya kihistoria namba 10 kuanzia msimu ujao kutoka 19 ya sasa, sambamba na mkataba mpya wa muda mrefu.

Jezi hiyo ina heshima kubwa ndani ya Barcelona na mara ya mwisho Lionel Messi aliivaa kabla ya kukabidhiwa Ansu Fati ambaye ameonekana kushindwa kuitendea haki.

Yamal, ambaye anamaliza msimu akiwa katika kiwango cha juu, alifunga bao la kuvutia lililowasaidia Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga dhidi ya Espanyol wiki iliyopita.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 17, alikuwa hatari kwenye mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan, ingawa juhudi zake hazikutosha kuwazuia Wataliano hao kuwanyima Barcelona nafasi ya kutwaa mataji manne msimu huu.

Kwa mujibu wa mfumo wa tathmini wa FlashScore, Yamal ametajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi katika mechi sita kati ya saba zilizopita za Barca, ikiwa ni pamoja na mikondo yote miwili dhidi ya Inter na fainali ya Copa del Rey dhidi ya Real Madrid.

Yamal tayari ametoa pasi za mabao 20 na kufunga mabao 18 msimu huu, Barcelona inaonekana iko tayari kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kijana huyo anaendelea kusalia klabuni hapo kwa muda mrefu zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti, Barcelona itampa Yamal mkataba mpya mnono utakaojumuisha kipengele kikubwa cha kuuvunja, pamoja na heshima ya kuvaa jezi namba 10. Ripoti hiyo inadai kuwa haijalishi nini kitaendelea kuhusu mustakabali wa Ansu Fati, tayari uamuzi umefanyika kwamba Yamal atavaa namba 10 kwa msimu wa 2025-26. Hii itamweka kwenye orodha ya heshima ya wachezaji waliowahi kuivaa jezi hiyo maarufu akiwemo Lionel Messi, Rivaldo, Gheorghe Hagi, Hristo Stoichkov na Diego Maradona.

Yamal atatimiza miaka 18 katikati ya mwezi Julai na mara tu atakapofikisha umri huo, Barcelona itasaini naye mkataba mpya wa muda mrefu utakaojumuisha kipengele cha kuuvunja cha euro bilioni 1.

Barcelona inaamini hatua hiyo itaashiria mwanzo wa enzi mpya ya mafanikio chini ya kocha Hansi Flick, ambaye msimu wake wa kwanza ameshinda mataji yote ya ndani Hispania.

Katika dili hilo, pia maanufaa ya nje ya uwanja yanatarajiwa kuongezeka, hasa katika mauzo ya jezi na mapato, huku mashabiki wakitarajiwa kumiminika kununua jezi zenye jina ‘Yamal 10’.

Wengi wanadhani uamuzi wa kumpa Yamal jezi ya namba 10 ni ishara ya mwisho kwa Ansu Fati klabuni hapo, ambaye amekuwa hana kiwango bora tangu kupewa jezi hiyo mwaka 2021 baada ya Lionel Messi kuhamia Paris Saint-Germain.

Fati ameanza mechi mbili tu msimu huu dhidi ya Mallorca na Valladolid, zote zikimalizika kwa yeye kutolewa mapema na kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha kwanza, hasa ikizingatiwa kuwa Raphinha yuko kwenye kiwango cha juu.

Kocha aliyepita, Xavi alikuwa hana imani na Fati, akamtoa kwa mkopo kwenda Brighton & Hove Albion msimu uliopita, lakini hata huko hakufanikiwa kung’ara.

Majeraha pia yamekuwa kikwazo kikubwa kwa Fati, ambaye msimu wa 2021-22 alikumbwa na jeraha kubwa baada ya kuanza vyema, na msimu huu pia amekumbwa na matatizo ya kiafya, akiwa amecheza mechi sita tu za La Liga.