Kwa Rashford pesa siyo shida, anataka tu kucheza

Muktasari:
- Kocha wa miamba hiyo ya Old Trafford alifichua sababu za kumwacha Rashford ni kutokana na kutokujituma mazoezini na haridhishwi naye.
WANASEMA ukiona cha nini wengine wanawaza watakipata line. Ndicho kilichotokea kwa Marcus Rashford ambaye alikuwa hapati namba kwenye kikosi cha Manchester United na zaidi hakujumuishwa kabisa kwenye michezo ya timu hiyo.
Kocha wa miamba hiyo ya Old Trafford alifichua sababu za kumwacha Rashford ni kutokana na kutokujituma mazoezini na haridhishwi naye.
Hata hivyo, wakati kocha huyo Mreno akikosa imani na Rashford, nyota huyo wa England ameibukia Aston Villa na jana alitarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Tottenham wa Kombe la FA na Kocha Mhispania Unai Emery anaamini atakiwasha kutokana na alivyomwona mazoezini.

Sasa unaambiwa nyota huyo aliye kwa mkopo Villa, wala hana presha kwani kuondoka Man United wala hakujamteteresha nje ya uwanja na maisha ndo yanazidi kuwa matamu kutokana na waleti yake na huku ni kwenda tu kupata changamoto mpya kisoka ili kulinda kipaji chake.
Kwa upande wa pesa, kwake siyo shida na ATM inakuchambulia namna nyota huyu anavyopiga pesa kwenye soka na nje ya soka na anavyozitumia ikiwamo kumiliki mali za maana yakiwamo magari ya kifahari.
ANAVYOPIGA PESA
Akiwa Man United alikuwa analipwa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki na ndiyo huo huo analipwa Villa aliko kwa mkopo, ikiwa ndiyo asilimia kubwa ya kipato chake.
Nyota huyu pia anapiga pesa kutokana na madili ya ubalozi na udhamini kutoka kampuni mbalimbali zikiwamo Coca-Cola, Chevrolet, Burberry na H&M inayojihusisha na mitindo na huuza mavazi ya bei nafuu.
Pia ana mkataba na kampuni inayomiliki migahawa ya McDonald pamoja na wa Nike inayomlipa kwa kuwa balozi wake.
Kutokana na madili hayo ya mikataba, anavuna takribani Dola 20 milioni kwa mwaka na hadi sasa anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 80 milioni.

NYUMBA
Mwaka 2021, alinunua nyumba ya kifahari yenye thamani ya Pauni 2.8 milioni huko Wilmslow, Cheshire yenye vyumba vitano vya kulala, chumba cha mazoezi, chumba cha sinema na bwawa la kuogelea la nje.
Rashford pia anamiliki nyumba yenye thamani ya Pauni 1.8 milioni huko Bowdon, Manchester, aliyoinunua mwaka 2019 na ina eneo la mazoezi, ukumbi wa sinema, chumba cha kuchezea game na bustani kubwa.

NDINGA
McLaren 765 Long Tail-Dola 382,000
Rolls-Royce Cullinan-Dola 355,000
Rolls-Royce Black Badge Wraith-Dola 750,000
Range Rover Velar-Dola 89,225
Mercedes C Class Coupe-Dola 48,437
Mercedes GLA 2020-Dola 38,239
Mercedes S Class Coupe-Dola 131,289
Mercedes-AMG A45 -Dola 52,415
Audi RS4 Avant-Dola 84,460
Mercedes-AMG G63-Dola 180,000
Mercedes-AMG GT63 S-Dola 170,000

MISAADA KWA JAMII
Kama sehemu ya mikataba yake na H&M, alizindua kampeni maalum kuhusu utoaji wa chakula na msaada kwa watoto wa jamii maskini.
Mwaka 2020, aliandika barua ya wazi kwa bunge la Uingereza akiwahimiza wanasiasa kuendelea na mpango wa kutoa chakula cha bure kwa watoto wenye uhitaji kutokana na janga la virusi vya corona.
Pia amekuwa akishirikiana na taasisi ya FareShare inayojihusisha na kutoa msaada wa chakula kwenda kwa watu wasiojiweza.

MAISHA BINAFSI NA BATA
Awali alikuwa katika uhusiano wa muda mrefu na Lucia Loi kabla ya kuachana mwaka jana na kuibukia kwa mrembo Grace Rosa Jackson ambaye pia waliachana Desemba mwaka jana. Kwa sasa haijaripotiwa ikiwa yupo katika uhusiano na mrembo yeyote.