Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa huyu Akram, wala tusidanganyane!

MASHABIKI wengi wa soka wanalikumbuka jina la Hassan Afif kutokana na boli alilotembeza katika michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) ya mwaka 1991.

Katika michuano ya msimu huo iliyofanyikia jijini Dar es Salaam, Afif alikuwa akiitumikia Simba kama kocha mchezaji na aliibeba timu hiyo kila alipokuwa akiingia uwanjani kipindi cha pili akitokea benchi kumpokea Ayoub Mzee na kuwachizisha mashabiki na wapenzi za Wekundu wa Msimbazi.

Haikushangaza Simba kufika fainali za michuano hiyo na kuwakutanisha na waliokuwa watetezi wa kombe hilo, SC Villa ya Uganda ya wakali kama Majid Musisi, Issa Sekatawa, Paul Hasule na wengine.

Katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), wenyeji Simba walitwaa ubingwa kwa kuifunga SC Villa kwa mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani na Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ na kocha mchezaji, Hassan Afif.

Afif ndiye aliyeasisti mabao mawili ya Mogella, kisha naye kufunga jingine na kuipa Simba taji ililoenda kulitetea visiwani Zanzibar mwaka 1992 kwa kuwachapa watani wao wa jadi Yanga kwa penalti 5-4 katika fainali nyingine kali iliyochezwa kwa dakika 120 na kuisha kwa sare ya 1-1.

Miaka mitano baadaye tangu Afif afanye maajabu ya kuisaidia Simba kubeba taji hilo la Kagame jijini Dar es Salaam, mshambuliaji huyo alimpokea mtoto wa kiume akiwa Qatar alikoweka maskani.

Ndio, Afif Mtanzania mwenye asili ya Somalia alizaliwa mjini Moshi, mwaka 1956 kisha kutimkia zake Qatar kumalizia soka lake na inaelezwa alioa mwanamke Myemen nchini humo aliyebahatika kupata naye watoto sita, wakiwamo wa kiume wawili, Ali na Akram aliyezaliwa mwaka 1996.

Akram kama ilivyo kwa kaka yake Ali wamerithi kipaji cha kusakata soka kama baba yao, Ali akicheza kama beki wa kushoto na alikuwa kwenye kikosi cha Qatar kilichobeba taji la kwanza la AFC Asian Cup akiwa sambamba na Akram anayecheza kama mshambuliji akimudu pia winga ya kushoto.

Alimudu pia kucheza kama kiungo mshambuliaji. Soka lake sio la kubahatisha ndio maana haikushangaza katika fainali za Kombe la Dunia 2022, Akram alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Qatar kilichokuwa wenyeji wa fainali hizo na kuishia hatua ya makundi.

Hakuna aliyemtilia maanani, hadi hivi karibuni alipoiongoza timu hiyo ya Qatar kunyakua ubingwa wa Fainali za Kombe la Asia 2023 kwa kuifumua Jordan kwa mabao 3-1, huku Akram akipiga hat trick ya aina yake akiipa nchi yake ya kuzaliwa taji hilo kwa mara ya kwanza.

Akram alifunga mabao matatu kwenye mchezo huo yote yakitokana na mikwaju ya penalti na kuiwezesha Qatar kubeba ubingwa wa fainali hizo, huku mwenyewe akiibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo akimaliza na mabao manane, akitangazwa pia Mchezaji Bora wa michuano hiyo ya 18.

CHA AJABU
Wakati Akram akiiwezesha Qatar kubeba taji hilo kwa msimu huu ikiwa ni mara ya pili kwake baada ya fainali za 2019, nchi ya baba yake mzazi, Tanzania ilikuwa imerejea siku chache zilizopita kutoka na kwenye ushiriki wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, zilizofanyika Ivory Coast.

Tanzania iling’olewa kwenye hatua ya makundi kwa kukusanya pointi mbili tu katika mechi tatu za Kundi F, ikifunga bao moja tu na kufungwa manne na kumaliza nafasi ya nne ya msimamo wa kundi hilo, lililoongozwa na Morocco na DR Congo zilizofuzu hatua ya 16 Bora.

Rudia tena, Stars imechezea mechi tatu za makundi na kufunga bao moja tu lililowekwa kimiani na Simon Msuva katika mchezo wa sare ya 1-1 dhidi ya Zambia, kwani ilifungwa 3-0 na Morocco na kulazimisha suluhu mbele ya DR Congo iliyomaliza kama mshindi wa nne wa fainali hizo ambazo wenyeji Ivory Coast walibeba taji kwa kuinyoosha Nigeria kwa mabao 2-1 katika fainali kali.

Taifa Stars ilishindwa kufurukuta, licha ya kukusanya wachezaji kadhaa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, wakiwamo walioletwa kutokana na kuwa na unasaba wa Kitanzania kama ilivyo kwa Akram aliyeamua kuitumikia Qatar kama taifa lake na sio Tanzania ya baba yake.

Unaweza kuwaza tu, iwapo Akram angeamua kufuata uraia wa asili ya baba yake na kuitwa Stars angetupa mafanikio gani?
Katika kikosi cha Stars kilichoenda Afcon 2023, kulikuwa na wachezaji aina ya Akram kama saba akiwamo kipa Kwesi Kawawa, mabeki Miano Danilo Van den Bos na Haji Mnoga, viungo washambuliaji Ben Starkie, Charles M’Mombwa, Tarryn Allarakhia na Mohammed Sagaf.   

Qatar walimuamini Akram na kumpa kazi na matunda yameonekana, hata kama ushindi ni wa timu nzima wa taifa hilo.
Akram hana tofauti na Yussuf Poulsen, nyota mwingine mwenye asili ya Tanzania, aliyeamua kuchukua uraia wa Denmark, licha ya asili yake kuwa hapo Tanga. Poulsen ni Mdigo kabisa, lakini siasa za soka la Tanzania zimemfanya achague Denmark taifa alilozaliwa na leo anakiwasha katika timu ya taifa ya nchi hiyo akiiwakilisha hadi katika fainali za Kombe la Dunia, huku tukiishia kummezea mate kwa uchu.

JUZI JUZI TU
Wakati leo tunawatolea macho na kutamani kina Akram na Poulsen wangekuwa wakiitumikia Stars, juzi kati tu tumeamua kuwafungia vioo kina Nestory Irankunda na Bernard Kamungo kwa sababu zilezile za siasa na miaka michache ijayo tujiandae tena kuwalilia na kuwamezea mate wachezaji hao.

Nyota hao waliozaliwa kwenye makambi ya wakimbizi pale Kigoma walitamani sana kuichezea Tanzania, lakini siasa zilizopo kwenye soka letu, zikawafanya wakinai kabla ya kuanza kuvaa uzi wa timu ya taifa.

Kamungo aliitwa kikosini Stars akaja, lakini akaishia kuwekwa jukwaani, kitu kinachoelezwa kilimkinaisha na kuzira akitulia zake katika klabu yake ya FC Dallas ya Marekani alikoitungua bao tamu timu ya Lionel Messi ya Inter Miami. Amechagua kuichezea mazima timu ya taifa ya Marekani iliyoamua kumkunjulia mikono kumpokea.

Tulikwama kwa Adam Nditi na wengine tukaishia kuwafungulia mkono kina Allarakhia wanaotoka madaraja ya chini zaidi barani Ulaya, tena baada ya kelele nyingi za mashabiki.

TULICHOSAHAU
Tumekuwa tukiweka siasa nyingi kwenye soka, letu huku tukisahau kama Mbwana Samatta umri unamtupa mkono. Tumesahau kwamba anakaribia miaka 30 na ile kasi yake imepungua.
Tumejisahaulisha kwamba, Simon Msuva naye anaelekea ukingoni na hatujaandaa wachezaji wa kurithi nafasi zao katika timu ya taifa.
Tunaendelea kuamini Samatta na Msuva wataichezea Stars kwa muda mrefu, hatujaandaa nyota wa wa kurithi kuanzia sasa wakiwamo wachezaji wenye asili ya Kitanzania wenye uwezo mkubwa na kiu ya kulitumikia taifa hili.

Tumeshindwa kuiga mataifa mengine kama Cape Verde, Comoro na mengineo wanaokusanya wachezaji wenye asili ya mataifa hayo wanaocheza Ulaya hasa nchi za Ufaransa ambao wamekuwa ni mtaji wa faida kwa timu za taifa za nchi hizo kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa.

Hata Ufaransa, ilitwaa taji la Fainali za Kombe la Dunia 1998 kwa kikosi kilichoundwa na wachezaji wenye uraia wa nchi za Kiafrika. Kwanini? Ni kwa sababu waliangalia zaidi vipaji na kuwapa uraia na matunda yameonekana, kwani hata fainali za 2018 ilipobeba tena taji hilo na zile za 2022 kikosi cha Ufaransa kilikuwa na wazamiaji wengi kuliko Wafaransa halisi.

NINI KIFANYIKE?
Kuna mambo mawili yanayoweza kufanywa ili kujiweka pazuri kwenye soka la kimataifa, ikizingatiwa tunajiandaa kuwa wenyeji wa Fainali za Afcon 2027 tukishirikiana pamoja na majirani zetu wa Kenya na Uganda.

Tanzania tunaweza kurejea upya na kuangalia sheria ya uraia pacha ambayo ndio inayotajwa kuwa kikwazo cha kupata wachezaji wenye viwango vya juu kuja kuichezea timu ya taifa.
Licha ya mara kadhaa serikali kukaririwa italiangalia hilo kwa jicho la ziada, lakini ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu na hivyo kuzidi kujinyong’onyesha wenyewe.

Kama hilo litarekebishwa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakuwa na kazi kubwa ya kuwasaka wachezaji wenye asili ya Kitanzania waliojazana Arabuni na Ulaya wanaocheza ligi mbalimbali ili kuja kuwatumia kwenye timu ya taifa na matunda yataonekana, kwani hata huyo Akram ambaye leo tunamtafakari, huenda angekuja kukipiga Tanzania, lakini tulishabugi mapema.

Lakini kubwa zaidi ni kutengeneza mpango kazi ambao utazalisha na kuendeleza nyota wenye vipaji tangu wakiwa wadogo ili kuja kurithi nafasi za mastaa waliopo sasa.