KUNA JAMBO… Salah kwa Slot atabaki tu

Muktasari:
- Slot ambaye amechukua mikoba ya Jurgen Klopp aliyedumu katika kikosi hicho kwa muda usiopungua miaka tisa alianza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha Liverpool mwanzoni mwa mwezi huu ambapo amefanya kazi na wachezaji kadhaa ambao hawakuwa sehemu ya timu zao za taifa katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
LIVERPOOL, ENGLAND: KIPA wa zamani wa Liverpool, Adrian amefichua kwamba mshambuliaji wa timu hiyo, Mohamed Salah amevutiwa sana na mbinu na mipango ya kocha mpya Arne Slot baada ya kufanya mazoezi na timu ndani muda mfupi tu hali inayoashiria kwamba anaweza akaendelea kuwepo licha ya tetesi kudai kwamba anataka kuondoka.
Slot ambaye amechukua mikoba ya Jurgen Klopp aliyedumu katika kikosi hicho kwa muda usiopungua miaka tisa alianza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha Liverpool mwanzoni mwa mwezi huu ambapo amefanya kazi na wachezaji kadhaa ambao hawakuwa sehemu ya timu zao za taifa katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
Kwa sasa ameanza kupokea kundi kubwa la mastaa wa kikosi cha kwanza ambao wamerejea katika timu baada ya kumaliza majukumu ya kuyatumikia mataifa yao katika michuano mbalimbali ikiwemo Copa America na Euro.
Adrian sio sehemu ya kikosi hicho baada ya kuachana na timu katika dirisha hili lakini bado amekuwa katika mawasiliano ya karibu na wachezaji wenzake wa kikosi cha kwanza ikiwemo Salah ambao amesema wamemwambia wanafurahishwa sana na mifumo pamoja na mbinu za kocha huyo.
Akizungumza na The Athletic, Adrian alisema: “Ninazungumza karibu kila siku na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza, kama Kostas Tsimikas na Mo Salah. Wananiambia kwamba wanapenda jinsi kocha huyo anavyofundisha, kuna baadhi ya vitu anafanana kabisa na Jurgen kama kucheza kwa nguvu, kwa kasi, kukabia juu, kuwa na ujasiri na kucheza moja kwa moja, hayo ni moja kati ya mambo kikosi cha Liverpool cha sasa kiliundwa nayo, hivyo naona kocha mpya anaenda katika njia hizo na niwatakie kila la kheri.’’
Inaelezwa kumekuwa na wasiwasi sana kwa mashabiki wa Liverpool juu ya Mohamed Salah wanaoona kuna uwezekano mkubwa staa huyo akaondoka katika dirisha hili kutimkia Saudi Arabia ambako alikuwa akiwindwa tangu msimu uliopita.
Mkataba wa sasa wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao na Al-Ittihad ambayo katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana iliwasilisha ofa ya Pauni 150 milioni ambayo ilikataliwa na Liverpool, bado inavutiwa.
Kwa sasa Liverpool inamshawishi Salah ambaye amefunga zaidi ya mabao 200 ya michuano yote tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2017 kusaini mkataba mpya lakini mazungumzo yanaonekana kugonga mwamba.
Inadaiwa kwamba Salah aligoma kuondoka msimu uliopita kwa sababu alihitaji kumaliza msimu chini ya Klopp ambaye ndiyo alikuwa anaondoka kisha baada ya hapo ndio aondoke ingawa kabla ya kufanya hivyo, alihitaji kuona mipango na kile ambacho kocha mpya baada ya Klopp angekuja nacho ndio yeye afanye uamuzi.
Kwa mujibu wa ripoti kuendana kimtazamo kati ya Klopp na Arne inaweza kuwa moja ya sababu zitakazochangia sana kwa Salah kubaki na kuichezea Liverpool msimu ujao na ikiwezekana akasaini kabisa mkataba mpya.
Changamoto kubwa ni kwamba kama Salah atabaki hadi mwakani bila ya kusaini mkataba mpya, Liverpool itakuwa na asilimia kubwa ya kumpoteza bure, hivyo inataka kumshawishi asaini mkataba mpya kabla ya mwaka kupinduka na kama ikishindikana inaweza kufikia uamuzi wa kumuuza.
Mbali ya Salah, mastaa wengine tegemeo ambao mikataba yao inaelekea ukingoni ni makapteni wa timu hiyo Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold ambao wanahusishwa kuwa katika mpango wa kuuzwa ikiwa hawatokubali kusaini dili mpya.