Kompyuta yaiondoa Arsenal kwa PSG

Muktasari:
- PSG haijawahi kushinda taji hili licha ya uwekezaji mkubwa ambao imekuwa ikiufanya kwa muda mrefu ikisajili mastaa kama Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe katika miaka ya hivi karibuni.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza wa mechi ya nusu fainali kwa bao 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Emirates dhidi ya PSG, Arsenal imetabiriwa kuwa na asilimia ndogo za kwenda kupindua matokeo na kufika fainali kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta maalum.
Arsenal ilipoteza mechi hiyo kwa bao la mapema la dakika ya nne lililofungwa na nyota wa PSG, Ousmane Dembele.
PSG haijawahi kushinda taji hili licha ya uwekezaji mkubwa ambao imekuwa ikiufanya kwa muda mrefu ikisajili mastaa kama Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe katika miaka ya hivi karibuni.
Kama ilivyo kwa PSG, vijana wa Mikel Arteta pia hawajawahi kushinda taji hili na hii ni nusu fainali yao ya kwanza tangu mwaka 2009.
Hata hivyo, kompyuta maalumu inayotumika kufanya utabiri imefichua kuwa Arsenal yenye maskani yake Kaskazini mwa London ina nafasi ya asilimia 12.7 tu za kushinda mashindano hayo.
Arsenal italazimika kuifunga PSG huko Ufaransa katika dimba la Parc de Princes kisha kuishinda timu moja kati ya Barcelona au Inter Milan ili kutwaa taji hilo.
Nafasi yao ya kugeuza matokeo ya nusu fainali kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta imekadiriwa kuwa asilimia 23.3 tu.
PSG imetajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda taji hilo, kwa asilimia 42.6.
Iwapo Luis Enrique ataiongoza PSG kutwaa taji hilo, itakuwa mara ya kwanza kwa klabu ya Ufaransa kushinda taji la michuano ya kimataifa tangu Marseille ilipofanya hivyo mwaka 2023.
Barcelona ni timu ya pili katika utabiri yenye uwezo wa kushinda taji hili ambapo imepewa nafasi ya pili nyuma ya PSG ikipewa asilimia 23.8, huku Inter Milan ikiwa na asilimia 20.9.