Kompyuta ya vituko! Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- Fainali hizo zitakazohusisha timu 32 zitafanyika huko Marekani na zitaanza, Jumapili Juni 15.
LOS ANGELES, MAREKANI: KOMPYUTA maalumu imetoa utabiri wa kushangaza wa mshindi wa Kombe la Dunia la Klabu litakalofanyika huko Marekani huku ikiitaja Chelsea itakomea kwenye hatua ya 16 bora.
Fainali hizo zitakazohusisha timu 32 zitafanyika huko Marekani na zitaanza, Jumapili Juni 15.
Kompyuta hiyo ya BoyleSports, imefanya uchambuzi wake kwa kuchezesha mechi 10,000 na kutoa matokeo yatakavyokuwa kwenye fainali hizo za Fifa kwa ngazi ya klabu.
Chelsea inapewa nafasi kubwa ya kuongoza kundi lake lenye timu za ES Tunis, Flamengo na Los Angeles FC. Lakini, kwa uchambuzi wa kompyuta hiyo, The Blues itamaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake, nyuma ya klabu hiyo ya Tunisia, ES Tunis.
Jambo hilo litaifanya timu hiyo inayonolewa na Kocha Enzo Maresca kukabiliana na Benfica kwenye hatua ya 16 bora, ambao watapenya kutoka kwenye kundi gumu lenye timu za Bayern Munich, Boca Juniors na Auckland City. Na matokeo ya kushtua yaliyotabiriwa na kompyuta ni Chelsea itachapwa 3-1 na miamba hiyo ya Ureno.
Kwa upande mwingine wa utabiri wa kompyuta hiyo ni Manchester City itamaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake lenye timu za Juventus, Al-Ain na Wydad Casablanca. Lakini, kikosi hicho cha Pep Guardiola kitaonyesha kiwango bora kwenye mechi za mtoano na itazitupa nje Real Madrid, Inter Milan na Juve kufika hatua ya fainali. Kompyuta inatabiri kwenye hatua ya fainali, Man City itamenyana na Benfica katika kipute kitakachopigwa Julai 13, New Jersey.
Matokeo yaliyotabiriwa kwenye mechi hiyo ya fainali ni Benfica itashinda 2-1 na kubeba ubingwa.
PSG ni kwamba itakwenda kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu ikiwa na uchovu wa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na itakomea kwenye hatua ya 16 bora, ikitupwa nje na Palmeiras.
Miamba hiyo ya Brazil, Palmeiras na wababe wa Argentina, River Plate ndizo timu zitakazokuwa kwenye viwango bora kabisa kwa upande wa Amerika Kusini, ambazo zote zitafika robo fainali.
Lakini, Botafogo nayo itakuwa kwenye makali mazuri, itapenya kwenye kundi lake badala ya Atletico Madrid. Matajiri wa Saudi Arabia, Al-Hilal watasonga mbele kutoka kwenye kundi lao litakalokuwa na vigogo Real Madrid, RB Salzburg na Pachuca, lakini itakwenda kukwama kwenye hatua ya 16 bora.
Kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta hiyo, Real Madrid, Man City, PSG na Bayern Munich, ambazo zimekuwa zikipewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua ubingwa, hazitakuwa na makali yoyote mbele ya Benfica ambayo ndiyo iliyotabiriwa itabeba taji hilo la kwanza la fainali za Kombe la Dunia la Klabu la Fifa.