Kocha mpya Man United, Tuchel kajitoa!
Muktasari:
- Bosi huyo wa zamani wa Chelsea, Tuchel alikutana mara mbili na mmiliki mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe wiki za hivi karibuni wakati tajiri huyo alipomfuata kujadili naye mpango wa kwenda kuinoa miamba hiyo ya Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Mjerumani Thomas Tuchel wala hataki kazi ya kwenda kuinoa Manchester United na amewaambia mabosi wa miamba hiyo ya Old Trafford kwa sasa anataka kujipumzisha kidogo na mambo ya soka.
Bosi huyo wa zamani wa Chelsea, Tuchel alikutana mara mbili na mmiliki mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe wiki za hivi karibuni wakati tajiri huyo alipomfuata kujadili naye mpango wa kwenda kuinoa miamba hiyo ya Old Trafford.
Man United ilimweka Tuchel namba moja kwenye chaguo lao la kocha wanayetaka akarithi mikoba ya Erik ten Hag huko Old Trafford wakati itakapoamua kuachana na Mdachi huyo.
Hata hivyo, baada ya kuachana na Bayern Munich kwenye majira haya ya kiangazi, Tuchel sasa anataka kujiweka mbali na mambo ya soka, akajipumzishe na presha za ukocha za wiki kwa wiki.
Na jambo hilo linamfanya kujiondoa kwenye mchakato wa makocha wanaohusishwa na mpango wa kwenda kuchukua mikoba ya Ten Hag, ambaye kwa sasa bado hajafahamu hatima ya maisha yake kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Kocha Tuchel aliweka wazi namna ya kwenda kumaliza matatizo ya Man United – ikiwamo kupata huduma bora kabisa kutoka kwa Jadon Sancho. Tuchel alitoa mfano wa beki wake wa zamani kwenye kikosi cha Chelsea, Antonio Rudiger, ambaye aliweza kumfanya Mjerumani huyo kuwa bora kabisa ndani ya uwanja kabla ya kubamba dili lake la kwenda kukipiga na Real Madrid.
Lakini, Ten Hag aliisaidia Man United kubeba taji la pili kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kunyakua Kombe la FA kwa kuichapa Manchester City kwenye mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Wembley.
Hata hivyo, zimeshafika wiki mbili hajafahamu hatima ya maisha yake kwenye kikosi hicho – ambapo bosi Ratcliffe na mabosi wenzake kwenye kampuni ya Ineos wamekuwa wakijaribu kuufanyia tathmini msimu wa Man United ulivyokuwa.
Man United haitakuwapo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2024/5 baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Kwenye hilo, kocha Ten Hag alitoa kisingizio cha kikosi chake kuandamwa na majeruhi wengi kwa msimu wote.
Bilionea Ratcliffe anafahamu wazi Ten Hag anapata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki – na sasa anakabiliwa na kasi ya muda katika kuweka michakato sawa katika kutambua mwelekeo wa klabu hiyo baada ya mambo ya msimu uliopita. Na sasa kinachoaminika uamuzi wa mwisho wa ama kubaki na Ten Hag au kumfungulia mlango wa kutoka na kuletwa kocha mpya utafanywa wiki hii.
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate ni mtu mwingine anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kumbadili Ten Hag huko Old Trafford – lakini kwa sasa yupo kwenye majukumu ya kikosi cha Three Lions kwenye Euro 2024 huko Ujerumani.
Graham Potter ni kocha mwingine kwenye orodha hiyo ya wanaotajwa huko Old Trafford. Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Brighton kwa sasa hana kazi tangu alipofutwa kazi huko Stamford Bridge. msimu uliopita.