Klopp simu moja tu Odegaard anatua Anfield

Thursday April 08 2021
klop pc

LONDON, ENGLAND: KIUNGO Martin Odegaard amewasha moto kwelikweli huko Arsenal anakocheza kwa mkopo na kupiga hesabu za kubaki Emirates, lakini kocha Jurgen Klopp akinyanyua simu yake tu na kumtaka aende Liverpool, fasta staa huyo wa Norwich anatua Anfield.

Odegaard amekuwa kwenye kiwango bora Emirates akitoka kwa mkopo Real Madrid na kuripotiwa kwamba huenda staa huyo huenda akanaswa jumla na Washika Bunduki hao wa London wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa.

Kiungo huyo wa Norway bila ya shaka ataruhusiwa kuondoka, hasa ukizingatia kwamba Los Blancos wanataka kuchangisha pesa kwa ajili ya kufanikisha usajili wa straika Erling Haaland.

Odegaard amekwenda Arsenal kuchukua mikoba ya Mesut Ozil na ndani ya muda mfupi tu ameonyesha kiwango bora kabisa na kujikusanyia mashabiki kutokana na kile anachokifanya ndani ya uwanja.

Kocha Mikel Arteta atahitaji huduma yake ya jumla, lakini sasa atakwenda kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England.

Kinachoelezwa ni kwamba Klopp amepanga kumnasa kiungo huyo baada ya kuzungumza naye Jumamosi iliyopita wakati Arsenal ilipokipiga na Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Advertisement

Gazeti la Hispania la AS limedai kwamba jambo hilo wala si uvumi, kwani Odegaard amekuwa akivutiwa na mpango wa kwenda kukipiga Anfield siku nyingi tu. Tangu kipindi hicho, akiwa anacheza kwao Norway, Odegaard alikuwa akisakwa na timu nyingi za Ulaya, lakini mwenyewe alisema anataka kwenda Liverpool.

“Liverpool siku zote imekuwa ni klabu ya ndoto zangu,” alisema Odegaard kwa wakati huo.

Kwa sasa bado ana mkataba wa miaka miwili huko Real Madrid, lakini yeye ni mmoja kwenye orodha ya wachezaji ambao wanaweza kufunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu. Wachezaji wengine wanaotajwa kwamba huenda wakapigwa bei na Los Blancos ni Gareth Bale, Brahim Diaz na Luka Jovic.

Advertisement