Klopp atajwatajwa huko Real Madrid

Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa Liverpool, Klopp alidai kwamba amechoka sana baada ya miaka tisa ya kuinoa timu hiyo ya Anfield, hivyo alihitaji muda wa kumpumzika, wakati sasa akiwa mkuu wa soka wa Red Bull Group, inayomiliki timu za RB Leipzig na RB Salzburg.
MUNICH, UJERUMANI: KIAPO cha Jurgen Klopp alichoweka ni kwamba atapumzika baada ya kuachana na Liverpool, lakini sasa kumekuwa na tetesi nyingi zikimhusisha na mpango wa kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Real Madrid.
Kocha huyo wa zamani wa Liverpool, Klopp alidai kwamba amechoka sana baada ya miaka tisa ya kuinoa timu hiyo ya Anfield, hivyo alihitaji muda wa kumpumzika, wakati sasa akiwa mkuu wa soka wa Red Bull Group, inayomiliki timu za RB Leipzig na RB Salzburg.
Lakini, sasa kumekuwa na uvumi mkubwa kwamba huenda akaibukia Madrid, licha ya Klopp kushikilia msimamo kwamba hatahitaji kazi ya ukocha kwa sasa. Real Madrid itaachana na kocha wake Carlo Ancelotti, ambaye ameripotiwa kwamba ataondoka Bernabeu mwishoni mwa msimu huu.
Straika wa zamani wa Liverpool, Peter Crouch na staa wa zamani wa Chelsea, Steve Sidwell walifichua kwamba kuna uwezekano mkubwa wa Klopp akaibukia kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kutangazwa kuwa kocha wa Real Madrid.
Crouch alidai kwamba kama Real Madrid itampelekea ofa Klopp hicho ni kitu ambacho hatakuwa tayari kukigomea, lakini Sidwell akiamini kwamba si kawaida kabisa ya kocha huyo kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
"Sidhani kabisa kama atahitaji kupumzika," alisema Sidwell.
"Mtazame Pep (Guardiola), nadhani walizaliwa kupambana. Wanahitaji kuanza upya wakihisi kuna vitu vimewatupa mkono."
Uvumi huo wa Klopp kwenda kuchukua mikoba ya Madrid umewekewa uzito na rafiki yake wa karibu, Miroslav Tanjga. Wawili hao waliwahi kucheza timu moja huko Mainz, na sasa Tanjga alisema kocha huyo Mjerumani kuna kazi mbili anazifukuzia.
"Klopp alichoniambia wakati anaondoka Liverpool ni kwamba alikuwa na ndoto mbili, kuinoa timu ya taifa na Real Madrid. Sijui kama ndoto zake hizo zitakwenda kutimia," alisema Tanjga.