Prime
BALAA! Tishio jipya afya za mastaa Ligi Kuu bara

Muktasari:
- Wakati ligi hiyo msimu huu ikiwa ukingoni, rekodi zinaonyesha zimeshapigwa mechi 35 mchana wa jua kali, huku timu 13 kati ya 16 zikiwa ndizo zimecheza mechi hizo.
LIGI Kuu Bara ipo ukingoni kabla ya kufikia tamati, huku zikiwa zimeshapigwa mechi 210 ikiwamo iliyochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kati ya wenyeji Simba na Mashujaa kutoka Kigoma.
Wakati ligi hiyo msimu huu ikiwa ukingoni, rekodi zinaonyesha zimeshapigwa mechi 35 mchana wa jua kali, huku timu 13 kati ya 16 zikiwa ndizo zimecheza mechi hizo.
Ni klabu tatu za Simba, Yanga na Azam ndizo pekee ambazo hazijawahi kucheza mchana katika ligi hiyo tangu ipate udhamini wa Azam Media ambayo ndio yenye haki ya matangazo ya mechi upande wa televisheni. Ligi hiyo inashika nafasi ya nne kwa ubora Afrika baada ya Misri, Morocco na Algeria.
Baadhi ya timu kati ya hizo 13 zimekuwa zikicheza mechi zinazopigwa kati ya saa 7:00 mchana hadi saa 8:00 mchana na kuendelea, tofauti na ilivyozoeleka nyingi kupigwa kuanzia saa 10:00 jioni hadi zile za usiku.
Takwimu zinaonyesha katika mechi 35 kati ya 210 zilizochezwa hadi sasa mchana , timu tatu za KenGold iliyoshuka daraja mapema ikiwa na michezo mitatu mkononi, Tanzania Prisons na Singida Black Stars ndizo zilizopigika juani, zikishuka uwanjani mara nane kila moja.

Pia Uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya ndio unaoongoza kwa kuchezwa mechi nyingi za saa 8 mchana kwani zimepigwa 12, huku wenyeji wa uwanja huo, KenGold na Tanzania Prisons kila moja ikicheza mara sita.
Timu hizo za Mbeya pia zimeshuka viwanja vya ugenini mara mbili kukabiliana na wapinzani wao majira ya saa 8 mchana na kukamilisha idadi ya mechi nane kwa kila moja.
Kwa Singida Black Stars yenye maskani yake mjini Singida ikitumia Uwanja wa Liti, mechi nane ilizocheza saa 8 mchana, tano imekipiga ikiwa nyumbani na tatu ugenini.
Idadi ya mechi za mchana inaweza kuongezeka iwapo mchezo wa Mei 13 kati ya JKT Tanzania na Fountain Gate utabaki kama ulivyopangwa awali na hivyo kufanya mechi kufikia 36, huku JKT na wapinzani wao wakiongeza idadi ya mechi.
Licha ya kuelezwa kwamba upangwaji wa ratiba kwa mechi za mchana kwa baadhi ya timu umejikita zaidi kwa ishu za kibishara kutoka kwa watangazaji wenye haki ya kurusha mechi hizo, lakini inaelezwa kuna athari ambazo hupatikana kwa wachezaji kucheza mchana wa jua kali, na wanaokosoa utaratibu huo wanaona klabu za nje ya Kariakoo na Mzizima tu ndizo zinazopangwa mchana.
Wajenga hoja wanasema hata Ulaya katika ligi kuu tano maarufu zipo mechi zinazogusa vigogo wa ligi hizo za England, Ufaransa, Hispania, Italia na Ujerumani zimekuwa zikipangwa mchana badala ya jioni na usiku ili kutoa uwiano sawa kwa timu zote, tofauti na hali ilivyo kwa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, inaelezwa kwa mechi za Ulaya kupigwa mchana wa saa 8 au saa 6 mchana, huwa ni mazingira na hali ya hewa ambayo ni ya baridi kulinganisha na Afrika Mashariki ambao ni ukanda wa kitropiki wenye hali ya hewa ya joto na wachezaji hutokwa jasho jingi.
Mbali na hayo, lakini inaelezwa kuwa kucheza kwenye joto kali huweza kusababisha ngozi kubabuka, kizunguzungu na hata wachezaji kuzimia kwa upotezaji huo wa maji na chumvi chumvi mwilini.

ATHARI ZAKE
Baadhi ya madaktari wa timu za Ligi Kuu Bara wamefichua kitendo cha kucheza mechi au kufanya mazoezi kipindi cha joto kali kuna madhara na kama wachezaji hawatapewa elimu ya kutosha, basi kuna hatari zaidi ya wengi wao kupata majeraha na matatizo mengine ya kiafya.
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo alisema: “Sababu kubwa ya hatari hiyo ni kutokana na mwili kupoteza maji na chumvi au madini mwilini kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida. Ndio maana kumekuwa na utaratibu wa wachezaji kutumia maji kwa wingi hasa kipindi cha joto kali.
“Endapo upotevu wa maji mwilini hautadhibitiwa ndivyo hatari ya athari hizo zinavyokuwa juu na pia kadri hali ya hewa ya joto inapozidi kuwa juu ndivyo maji hupotea zaidi mwilini.”
Kagabo alisema kawaida mwili huhitaji maji na chumvichumvi kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi seli.
“Wachezaji ambao wamekuwa wakicheza mechi katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali wanatakiwa kunywa maji mengi lakini pia wazungumze na waamuzi ili kuwazingatia kwa kuwapa mapumziko ya mara kwa mara ili waweze kunywa maji ya kutosha kuepusha shida ambazo zinaweza kuwapata.
“Kuvuja jasho sana huwa ni zaidi wakati wa kucheza katika joto kali na wakati huohuo kadri jasho linavyotoka kwa wingi na ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo tu mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kuvuja jasho.
“Mara nyingi wachezaji ambao wanapata madhara haya kirahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha kabla ya mechi na vilevile kutokula vyakula vyenye maji na madini ikiwamo matunda na mboga.
“Madini chumvi kwenye mwili wa binadamu ni muhimu sana na hasa kwa wachezaji ambao wanafanya kazi ambayo inawatoa jasho jingi hivyo wakikosa hayo wanaweza kupoteza fahamu lakini pia anaweza akapata degedege,” alisema Dk Kagabo.
“Lakini pia wachezaji wanapata shida ya kuchanika nyama za paja na misuli kukaza kutokana na kukosa baadhi ya madini muhimu ambayo yanaondoka mwilini kwa njia ya jasho.”
Alisema hali hiyo kiafya imekuwa ikichangia pia wachezaji kuumia na kubana kwa makundi ya misuli ikiwamo ile ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji kama wa soka.
Kagabo alisema madhara mengine yanayoweza kutokea kutokana na hali ya kutokwa sana na jasho na kupungiwa maji mwilini ni pamoja na kichwa kuuma, kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini mazoezini au mchezoni, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma na mwili kuuma.
“Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango bora hasa kukiwa na ratiba ngumu ya mechi mfululizo kwa sababu hawarudi haraka kwenye utimamu kutokana na kupoteza nguvu kazi nyingi kwa mchezo mmoja.”

Kwa upande wa Daktari wa KenGold, Amina Turusa alisema: “Ukiona mchezaji baada ya mechi ya mchana ambayo huchezwa kwenye jua kali amepata changamoto zozote, basi tambua huyo alikuwa na matatizo mengine ya kiafya mwilini mwake, ila tofauti na hapo hakuna athari zinazoweza kumpata.”
Dk Amina alisema kwa mechi zinazochezwa katika jua kali madaktari hushauriana na waamuzi kuweka muda maalumu wa kupumzika kwenye vipindi vyote viwili ‘cooling break’ ili kutoa nafasi kwa wachezaji kunywa maji kutokana na jasho linalowatoka.
“Suala la kucheza kwenye viwanja vyenye nyasi bandia katika jua kali athari zake zinazoweza kutokea ni majeraha madogo madogo ambayo husababishwa sana na aina ya viatu ambavyo mchezaji anatumia kutokana na kuungua miguu japo sio kwa wote,” alisema.
MAENEO YA BARIDI FRESHI
Kwa upande wa Daktari wa Fountain Gate, Shaaban Shija alifafanua zaidi kwa kusema: “Huku kwetu Babati mkoani Manyara ni sehemu ya baridi. Sasa unapoenda mkoa mwingine wenye mazingira tofauti na unapotoka ni lazima uchukue tahadhari ya kuhakikisha unawahi siku tatu zaidi kabla ya mechi hiyo husika.”
Shija alisema kucheza katika jua kali na uwanja ambao ni wa nyasi bandia mchezaji anachopaswa kuzingatia ni kutotumia viatu vyenye meno ya chuma, kwa sababu inaweza kumsababishia majeraha mbalimbali.
“Shida iliyopo kuna baadhi ya wachezaji hawana uelewa wa jinsi ya kutumia viatu kutokana na aina ya mazingira yenyewe, ndio maana wengi wao wanakutana na majeraha ambayo unaweza kusema ni ya kujitakia kwa sababu hawafuati taratibu husika.”
MAKOCHA, VIONGOZI
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Amani Josiah alisema kilichochangia wao kucheza kwa presha hadi sasa ni kutokana na ratiba ilivyobana na miundombinu si rafiki, kwani walikuwa wanatumia basi ambalo halikuwa zuri tofauti na walilonalo kipindi hiki.
“Kuhusu kucheza juani kwa Mbeya siyo ishu kwani hali ya hewa ni baridi, ila maeneo ya Pwani ni changamoto kwani tulikuwa tunakosa muda wa kuzoea mazingira kutokana na kubana kwa ratiba, miundombinu haikuwa rafiki, usafiri wetu ni wa basi na siyo ndege,” alisema.
Kocha wa KenGold, Omary Kapilima alisema mechi za mchana ni tatizo inabidi viongozi wa mamlaka husika waliangalie kutokana na wachezaji kuvuja jasho jingi, ingawa halihusiani na wao kupata matokeo mabaya.
“Mfano mechi ikichezwa saa nane mchana, maandalizi yanaanza saa sita, hivyo wachezaji wanakuwa wanatoa sana jasho na uchovu unakuwa mwingi,” alisema Kapilima ambaye timu anayoinoa imeshuka daraja.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabit Kandoro, alisema: “Mechi za saa 8:00 mchana kiuhalisia ngumu hasa kwa timu zinazosafiri umbali mrefu wachezaji wanakosa muda wa kupumzika, hivyo miili yao inakuwa haifunguki ni kama inapunguza ufanisi wao.

“Mfano mechi ambayo tulitoka Bukoba kwenda kucheza Mbeya dhidi ya Prisons tulitumia gharama kubwa wachezaji kuwa sawa lakini mwili wa binadamu kama haupo sawa haudanganyi, ingawa walijitahidi kwa kadri wawezavyo, naamini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ina watu makini italifanyia kazi jambo hilo, ingawa nisisitize halihusiani na kukosa matokeo mazuri.”
BODI YA LIGI
Kwa upande wa Bodi ya Ligi inayosimamia mechi za Ligi Kuu imetoa ufafanuzi, upangaji wa ratiba huhusisha wenye haki ya matangazo ambao wana vigezo vyao kwa lengo la kibiashara timu zipi zipangwe mechi zao kwa muda gani.
“Ukweli ni kwamba ratiba hupangwa kwa ushirikiano baina ya Bodi na wadhamini wenye haki ya matangazo kwa lengo la biashara kwa uwekezaji waliouweka katika udhamini, kuna timu zinauzika sana kuliko nyingine, ndio ukweli,” alisema kwa ufupi Steven Mnguto ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.
Hata hivyo, msimu uliopita wakati Geita Gold na Tabora United walipokuwa wahanga wa kucheza mechi nyingi za mchana ambazo zilichangia kupata matokeo mabaya, ikiwamo Geita kushuka daraja moja kwa moja sambamba na Mtibwa Sugar na Tabora kunusurika katika play-off, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Karim Boimanda, alikaririwa akisema tatizo kubwa ni uhaba wa viwanja vyenye taa ambavyo vingesaidia mechi nyingi kupigwa usiku.
Kwa sasa viwanja vyenye taa na vinavyotumika kwa mechi za usiku ni Majaliwa mkoani Lindi, Kaitaba mjini Bukoba, Jamhuri wa jijini Dodoma, Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar, Mkwakwani uliopo Tanga, ukiacha Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliopo jijini Dar es Salaam.
“Kuna changamoto ya upungufu wa viwanja vyenye taa, hii imechangia kwa kiasi kikubwa kwa ratiba ya kucheza mchama kuzibana baadhi ya timu,” alikaririwa Boimanda na kuongeza.
“Lengo ni kuona mechi zote zinaonyeshwa kwa mujibu wa mdhamini wetu wa haki ya matangazo, ila idadi ya viwanja hivyo vyenye taa, unachangia. Tunapopanga mechi za mchana pia tunaangalia hali ya hewa. Inapotokea inatengenezwa ratiba tunazingata saa 8 mchana ya Mbeya haiwezi kuwa sawa na Dar es Salaam.”
Pia alifafanua kwamba msimu huu, Bodi ingepanga mkakati wa kuongeza idadi ya viwanja vitakavyofaa kutumika kwa mechi za usiku lakini pia kuzungumza na wadhamini wa ligi hiyo, ili kupambana kwa jambo hilo kwa lengo la kuzisaidia timu na kuepuka haya malalamiko ya kila mara.
AZAM TV
Kwa upande wa Azam ambao ndio warushaji wa mechi za Ligi Kuu Bara kupitia televisheni, mkuu wa Kitengo cha Michezo, Philip Cyprian anasema ligi yoyote hasa mwishoni mwa wiki huwa na ratiba ya mechi kila wakati kuanzia mchana mpaka usiku.
Anasema watu wanafurahia mechi siku za mapumziko ndio maana wanapanga kuanzia saa 8 hadi 10 ili kupata watazamaji zaidi.
“Ligi kama za nje (Ulaya) wanakuwa na mechi mpaka saa 7 mchana, wengine hadi usiku kabisa, lakini ratiba hizo zinapangwa kutokana na hali ya hewa, lakini pia wingi wa watazamaji. Sisi watu ambao tuko upande wa kurusha mechi tunafurahia ratiba ya kuwa na mechi muda wote kwa sababu tunapata watazamaji kuanzia mchana mpaka usiku.
“Japokuwa kila muda una faida na hasara zake, mechi za mchana huwa zinatoa video yenye ubora wa kawaida kidogo kwa sababu ya mwanga wa jua, lakini hata kwa wachezaji inawafanya wapumzike sana kwa kunywa maji.
“Lakini pia ratiba za mchana kwa ligi yetu mara nyingi zinakuwa mikoani, mahali ambapo hali ya hewa yake inaruhusu kucheza muda huo, mfano Mbeya saa 7 au 8 bado kuna jua na baridi pia,” anasema Philipo.

NINI KIFANYIKE?
Dk Shita Samwel ambaye ni mchambuzi wa Kona ya Spoti Dokta inayotoka kila Alhamisi ndani ya Gazeti la Mwanaspoti, anafafanua juu ya kitu gani kifanyike kwa mazingira ya wachezaji wanaocheza mechi za mchana wa jua kali.
Dk Shita anasema wachezaji wanywe maji mengi siku mbili kabla ya mechi ikiwezekana lita 3 hadi 5 za maji kwa siku. Unywaji maji uwe ni utamaduni wa wakati wote kwa wachezaji na sio wakati wa joto pekee. Kwa watu wa kawaida glasi 8 hadi 10 kwa siku zinatosha kukabiliana na upungufu wa maji mwilini kipindi cha joto kali.
Anasema wachezaji wasisubiri kiu iwabane ndipo unywe maji na yanywewe mara kwa mara au kunywa kidogo mpaka ufikie lengo linalotakiwa. Vilevile kula matunda kwa wingi kila baada ya mechi na katika mlo tumia mbogamboga kwa wingi. Matunda na mboga huwa na maji mengi na madini (chumvichumvi).
Ni muhimu mchezaji akatambua umuhimu wa kunywa maji ya kutosha kabla ya kuingia mazoezini au katika mechi na vilevile kunywa maji kila baada ya nusu saa au wakati wa mapumziko na baada ya kumaliza mazoezi au mechi. Sio vibaya kwa klabu zenye uwezo kutumia vinywaji maalumu kwa ajili ya wanamichezo ambapo ndani yake huwa na wanga na chumvichumvi. Vinywaji hivi kama vinavyojulikana sports drinks ni muhimu kutumia.
Kwa faida ya wote, vinywaji vya kuongeza nguvu na kusisimua au kuchangamsha mwili maarufu kama energy drinks sio sahihi kutumia kwa mtu kuongeza maji mwilini. Pia pombe, soda na kahawa sio mbadala wa maji yaliyopotea kwa njia ya jasho.
Kipindi hicho wachezaji waepuke kukaa au kutembelea maeneo yenye joto na msongamano, badala yake wakae maeneo ya wazi yenye vivuli hasa kabla ya mechi. Ni muhimu kuupumzisha mwili kwa kulala angalau saa nane kwa siku.
Kama joto litakuwa ni kali sana ni vizuri kucheza wakati wa joto au jua kali linapokuwa limepungua kuaepushia wachezaji matatizo.
Ni vizuri kutoa mapumziko ya katikati ya mechi ili kutoa nafasi kwa wachezaji kunywa kiasi kidogo cha maji ili kukabiliana na hali hiyo. Joto hili ni tishio kwa wachezaji, ni vizuri watoe taarifa mapema kwa madaktari wa timu mara tu wanapopata dalili na viashiria vya madhara ya joto.