Prime
Chamou atibua hesabu Simba

Muktasari:
- Muivory Coast huyo ambaye alitua Simba msimu huu, alikuwa hana mwanzo mzuri kutokana na Che Malone na Hamza kuwa na uwezo mkubwa uliomshawishi kocha Fadlu muda mwingi kuwatumia.
KAMA utani hivi, beki wa kati Simba, Chamou Karaboue amebadili uamuzi wa mabosi wa klabu hiyo kutokana na kiwango chake, huku kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids akisema amefanikiwa kuwapa changamoto Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza.
Muivory Coast huyo ambaye alitua Simba msimu huu, alikuwa hana mwanzo mzuri kutokana na Che Malone na Hamza kuwa na uwezo mkubwa uliomshawishi kocha Fadlu muda mwingi kuwatumia.
Mwanaspoti linafahamu kuwa kabla ya Che Malone kuumia miezi ya karibuni, Simba ilikuwa inafikiria kusajili beki wa kati mwigine wa kigeni na kuachana na Muivory Coast huyo, lakini kiwango alichoonyesha Chamou kimebadilisha mtazamo wa benchi la ufundi na hata mabosi.
Chanzo ndani ya Simba zkimelidokeza Mwanaspoti kuwa: “Baada ya uwezo mkubwa aliouonyesha, mabosi wakaona hakuna sababu ya kusajili beki wa kigeni kwani raia huyo wa Ivory Coast anatakiwa kuendelezwa tu.
“Sasa wameamua kuendelea kumpa namba hata awe anapishana na wenzake kuliko kutokucheza kabisa kama kipindi kile.”
Fadlu amemzungumzia Chamou akisema beki huyo ameonyesha uwezo mkubwa kwenye mechi ambazo amecheza na kwa sasa amemtaka kuendelea kuwapa changamoto wenzake.
“Chamou ameonyesha uwezo mkubwa hasa katika utulivu, nguvu na matumizi ya akili nyingi anapokuwa uwanjani.
“Kwenye mechi ambazo amecheza mpaka sasa nataka awape changamoto zaidi Malone na Hamza ndani ya kikosi cha Simba,” alisema Fadlu.
Wakati huohuo, Kocha Fadlu amesema kwa sasa ndani ya kikosi hicho amepata matumaini mapya baada ya kurejea kwa viungo wake mahiri, Fabrice Ngoma na Charles Jean Ahoua.
Wawili hao wamekosekana katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Mashujaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeraha.
“Tunatumai tutawapata Ngoma na Ahoua mapema, tunahitaji kuwapumzisha wengine. Tumetoka kucheza mechi ngumu Afrika Kusini, tukaja hapa tukakutana na mchezo mwingine mgumu. Mabadiliko haya ya haraka yanahitaji mzunguko mzuri wa wachezaji,” alisema Fadlu.
Ahoua mwenye mabao 12 na asisti saba katika Ligi Kuu Bara msimu huu, pengo lake lilionekana kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa kutokana na mbadala wake, Awesu Awesu kushindwa kuonesha uthabiti wa kutosha hasa katika utengenezaji wa nafasi.
Kwa upande wa Ngoma, naye amekuwa kiungo muhimu eneo la ulinzi kutokana na uzoefu wake wa kucheza mashindano makubwa ya Afrika.
Katika mchezo dhidi ya Mashujaa, Simba ilionekana kukosa ubunifu hasa kipindi cha kwanza ambapo iliruhusu bao la mapema dakika ya tano kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi. Fadlu hakusita kueleza kwamba ilikuwa ni pengo la sekunde chache za kutokuwepo makini.
“Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza. Tulitengeneza nafasi, lakini tukaruhusu bao kwa sababu ya kukosa umakini. Baada ya hapo, Mashujaa walivunja mdundo wa mchezo kwa makusudi kupoteza muda, kipa kuanguka mara kwa mara, hatukuweza kuingia kwenye ‘rhythm’ yetu,” alisema.
Kwa sasa, Simba inaendelea na maandalizi ya mchezo mwingine wa ligi dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa kesho Jumatatu, Fadlu anaamini itakuwa mechi nyingine ngumu zaidi msimu huu.