Prime
Huyu ndiye aliyeamua shauri la Yanga CAS

Muktasari:
- Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ilianzishwa mwaka 1984 ili kutatua migogoro inayohusiana na michezo kwa njia ya usuluhishi. Makao yake makuu yako Lausanne, Uswizi na mahakama zake ziko New York City, Sydney, na Lausanne.
Jana Alhamisi, Mei Mosi, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ilitoa taarifa ya kufuta na kutoendelea na shauri lililofunguliwa na Yanga kuhusu mchezo wake wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ulioahirishwa dhidi ya Simba, Machi 8, 2025.
Yanga iliiomba CAS mechi ya marudiano baina yao na Simba isipangiwe tarehe na pia ipewe pointi za mezani.
Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu lakini ikaahirishwa baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku moja kabla ya mchezo.
CAS imeamua kutupilia mbali shauri hilo kwa vile Yanga haikufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko yake kwa kupeleka shauri hilo CAS kabla ya kuanza na vyombo vya ndani.

Jopo la majaji walioamua shauri hilo limeongozwa na makamu wa Rais wa Kitengo cha Usuluhishi wa Rufaa cha CAS, Elisabeth Steiner.
Steiner raia wa Austria aliyeongoza undeshaji na utoaji uamuzi kuhusu shauri hiyo ni gwiji wa masuala ya sheria na hilo linathibitishwa na wasifu wake.
Elisabeth (56) alizaliwa Machi 21, 1956 jijini Vienna, Austria na ana uwezo mzuri wa kuzungumza lugha za Kijerumani, Kiingereza na Kifaransa.
Amewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu akiitumikia kuanzia Novemba Mosi, 2001 hadi Oktoba 31, 2015.

Ana shahada ya uzamivu (PhD) ya masuala ya sheria aliyoipata mwaka 1981 lakini pia anayo nyingine ya usimamizi wa biashara aliyopata mwaka 1985.
Elisabeth amekuwa mjumbe wa kamati ya wataalamu wa sheria ya kazi ya Chama cha Wanasheria wa Vienna na vyama mbalimbali vya wanasheria wa kimataifa.
Aliteuliwa kuwa miongoni mwa majaji wa CAS mwaka 2019, mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Mfuko wa Kimataifa wa Wanawake upande wa Austria.
Tamko la TPLB
Muda mfupi baada ya CAS kuamua hilo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kujiandaa kupanga tarehe ya mechi hiyo.
“Манакама ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imetupa rufani ya klabu ya Yanga yenye kumbukumbu namba CAS 2025/A/11298 ambayo klabu hiyo iliifungua dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC).
“Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ambapo pamoja na mengine, klabu ya Yanga iliomba mechi tajwa hapo juu isipangiwe tarehe mpaka litakapotolewa uamuzi, ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (PLB), na klabu ya Simba.
“Kutokana na uamuzi huo wa CAS, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaendelea na maandalizi yake ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/2025 na kufanya maboresho ya ratiba ya Ligi (ukiwemo mchezo namba 184 - Young Africans vs Simba SC) kisha kutangaza ratiba mpya mapema iwezekanavyo,” imefafanua taarifa ya TPLB