Prime
Sababu tatu zilizoiangusha Yanga CAS

Muktasari:
- Aliyekuwa mkuu wa kitengo cha sheria wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick amewataka wana Yanga kuendelea kuwaunga mkono viongozi wao akidai wanapitia wakati mgumu.
MABOSI wa Yanga inaelezwa jana waliitana na kujifungia ili kujadili hukumu ya kesi waliyoifungua Mahakama wa Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (CAS), iliyotupiliwa mbali, huku zikitajwa sababu tatu zilizosababisha kesi kufutwa na ushauri waliopewa mabosi hao wa Jangwani.
Yanga ilikimbilia CAS baada ya mechi ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba kuahirishwa saa chache kabla ya kufanyika Machi 8, mwaka huu, ikidai kanuni za ligi zilikiukwa kimakusudi ili kuinufaisha Simba iliyotangaza isingecheza kwa kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Kwa Mkapa na mabaunsa wanaodaiwa kuwa wa Yanga. Hata hivyo, juzi hukumu ya kesi hiyo ilisambaa mtandaoni ikielezwa imefutwa na Bodi ya Ligi kutoa taarifa kuwa ilikuwa ikijianda kutoa ratiba mpya ya pambano hilo na mengine yaliyobaki ya ligi iliyosaliwa na raundi tatu kabla ya kufikia tamati. Mapema jana asubuhi ilielezwa mabosi wa Yanga waliitana ili kujadili na walikuwa wakijiandaa kutoa taarifa ya klabu, lakini mwanasheria na mwandishi mzoefu wa habari za michezo, Wakili Alloyce Komba aliyewahi kuwa wakili wa Yanga enzi za Yusuf Manji ametaja sababu tatu za kesi hiyo kufutwa na kwamba kila kitu kimeshaisha na Yanga iendelee na mambo mengine tu kwa sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Komba alisema kesi ya Yanga haipo kwa sababu kuu tatu ambazo alizitaja kuwa ni CAS imekosa mamlaka ya kusimamia kesi hiyo, kukosa hukumu iliyoifanya Yanga kukimbilia CAS na kushindwa kukamilisha mchakato kwa kufuata utaratibu.
“Kuna ngazi zimerukwa, hivyo CAS wamegundua kanuni ya TFF Ibara ya 26.26 au ukianzia 22 kuna kamati ya rufaa na Yanga haikuanzia huko kwa kufuata mchakato na badala yake wamekwenda moja kwa moja kule,” alisema Komba na kuongeza: “Hakukuwa na uamuzi ambao umetolewa na Bodi ya Ligi na TFF ambao uliifanya Yanga wakate rufaa hukumu waliyokuwa nayo ni kuahirishwa kwa mchezo ambayo imekataliwa na CAS, lakini pia walikuwa na malalamiko ya matumizi ya fedha huku wakiwa hawana viambatanisho.”
Alisema kwa mantiki hiyo Yanga haina kesi ya kusikilizwa na kuhusu kurudi haoni kama kutakuwa na nafasi kwa sababu kuna ukomo wa kusikiliza kesi za aina hiyo kwa kujaribu kurudi kufuata utaratibu.
Komba alisema Yanga inachotakiwa kufanya ni kufuata utaratibu itakaopewa na Bodi ya Ligi hasa kwenye mchakato wa kupokea maelekezo na kutekeleza. “Lakini, Yanga inatakiwa kulinda heshima na rais wa klabu hiyo, Hersi Said ambaye ni kiongozi mkubwa wa CAF wanamuweka kwenye hatari.”
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah, alisema kilichotokea kwa Yanga ni kutokana na Kamati ya Kusimamia na Kuendesha Mashindano ya Lihi kupewa mamlaka makubwa ya kutoweza kupingwa baada ya kufanya uamuzi wowote.
“Wakati tunaanzisha hii kamati ilikuwa imelenga kupitia na kusimamia kile kinachoripotiwa na waamuzi ndani ya dakika 90 za mechi, lakini imebadilishwa na kupewa majukumu makubwa yasiyopingwa na hivyo, Yanga iliamua kukimbilia CAS,” alisema Angetile.
“Kwa kawaida maamuzi yanayofanywa na chombo cha juu, haiwezekani tena kuanzishwa mchakato mpya juu ya kesi husika. Najua Yanga imejifungua kujadili hukumu, lakini kwa ushauri wangu ingeachana nayo na kukubali kucheza dabi, kwani timu yoyote ina nafasi ya kushinda.
“Ninachojua Yanga imefanya ilichokifanya kutaka kukumbusha mamlaka juu ya umuhimu wa kuzingatia kanuni na kuzitekeleza bila upendeleo au kuegemea kwa baadhi ya klabu.
“Ukifuatilia Simba ilitoa tishio la kutocheza na kusema ising-echeza ligi hadi waliohusika kuwazuia kufanya mazoezi waadhibiwe. Cha ajabu hadi leo waliohusika hawajaadhibiwa na Simba imecheza mechi za ligi ikiwamo ya jana. Hii ni kuonyesha haikuitaka dabi na Bodi iliingia kwenye mfumo wao.”
Angetile alisema anadhani baada ya msimu kumalizika Yanga ihamasishe klabu nyingine kuibana Bodi ya Ligi kusimamia kanuni inazoziweka na kwa vile rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ni mwenyekiti wa klabu za soka Afrika, anaweza kujifunza kupitia ligi zingine kuona jambo hilo halijirudiii tena.
“Kwa msingi huo ni kwamba mashabiki kwa sasa wanasikilizia juu ya ratiba mpya ya Dabi ya Kariakoo ambayo Yanga ilitishia kuicheza kwa madai ilistahili kupewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu kwa watani wao kuigomea mapema kabla ya Bodi kutoa tamko la kuiahirisha,” alisema.
ALIYEFUTA SHAURI CAS
Juzi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ilitoa taarifa ya kufuta na kutoendelea na shauri lililofunguliwa na Yanga kuhusu mchezo wake wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ulioahirishwa dhidi ya Simba, Machi 8, 2025.
Yanga iliiomba CAS mechi ya marudiano na Simba isipangiwe tarehe na pia ipewe pointi za mezani.
Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu lakini ikaahirishwa baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku moja kabla ya mchezo. CAS imeamua kutupilia mbali shauri hilo kwa vile Yanga haikufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko yake kwa kupeleka shauri hilo CAS kabla ya kuanza na vyombo vya ndani.
Jopo la majaji walioamua shauri hilo limeongozwa na makamu wa Rais wa Kitengo cha Usuluhishi wa Rufaa cha CAS, Elisabeth Steiner.
Elisabeth, raia wa Austria aliyeongoza uendeshaji na utoaji uamuzi kuhusu shauri hilo ni gwiji wa masuala ya sheria na hilo linathibitishwa na wasifu wake.
Elisabeth (56) alizaliwa Machi 21, 1956 jijini Vienna, Austria na ana uwezo mzuri wa kuzungumza lugha za Kijerumani, Kiingereza na Kifaransa. Amewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu akiitumikia kuanzia Novemba Mosi, 2001 hadi Oktoba 31, 2015.
Ana shahada ya uzamivu (PhD) ya masuala ya sheria aliyoipata mwaka 1981 lakini pia anayo nyingine ya usimamizi wa biashara aliyopata mwaka 1985.
Elisabeth amekuwa mjumbe wa kamati ya wataalamu wa sheria ya kazi ya Chama cha Wanasheria wa Vienna na vyama mbalimbali vya wanasheria wa kimataifa.
Aliteuliwa kuwa miongoni mwa majaji wa CAS mwaka 2019, mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mfuko wa Kimataifa wa Wanawake upande wa Austria.
TAMKO LA TPLB
Muda mfupi baada ya CAS kuamua hilo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kujiandaa kupanga tarehe ya mechi hiyo. “Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imetupa rufani ya klabu ya Yanga yenye kumbukumbu namba CAS 2025/A/11298 ambayo klabu hiyo iliifungua dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC).
“Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ambapo pamoja na mengine, klabu ya Yanga iliomba mechi tajwa hapo juu isipangiwe tarehe mpaka litakapotolewa uamuzi, ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (PLB), na klabu ya Simba.
“Kutokana na uamuzi huo wa CAS, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaendelea na maandalizi yake ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/2025 na kufanya maboresho ya ratiba ya Ligi (ukiwemo mchezo namba 184 - Young Africans vs Simba SC) kisha kutangaza ratiba mpya mapema iwezekanavyo,” imefafanua taarifa ya TPLB.
AELEZA MAZITO
Wakati sakata la Dabi ya Kariakoo likiendelea, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha sheria wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick amewataka wana Yanga kuendelea kuwaunga mkono viongozi wao akidai wanapitia wakati mgumu.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Patrick amesema kwa sasa anabaki kuwa mwanachama mtiifu wa Yanga. “Vita dhidi ya wahuni haijawahi kuwa rahisi. Wana Yanga wenzangu, najua maamuzi madogo ya CAS yamewaumiza, ila tuwapongeze viongozi wetu kwa kupinga uhuni kwa vitendo na nina uhakika hawajakata tamaa,” alisema Patrick aliyejiuzulu tangu Agosti 2024.
“Najua hawawezi kujitokeza kuwaeleza wanayoyapitia nyuma ya pazia, ila ipo siku mtawaelewa. Niwaombe wana Yanga muendelee kuwapa moyo na kuwaunga mkono kwa nguvu. Kwa muda niliotumikia klabu, nimejionea jinsi ilivyo changamoto kuiongoza klabu ya Yanga.
“Mwisho, nitumie fursa hii kuwaomba radhi ndugu zangu waandishi wa habari. Nimekuwa sipokei simu zenu, si kwamba sipendi kuzungumza nanyi, bali kwa sasa mimi ni mwanachama mtiifu wa Yanga. Nawaombeni mniruhusu niendelee kupumzika soka la Bongo, Yanga ina watu makini wengi na wenye weledi tuwape muda waendelee kutupambania.”