Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitaumana NBA mtoko wa Krismasi

Muktasari:

  • LeBron, Kevin Durant na Curry kwa pamoja ndio walichangia ushindi mgumu wa timu yao ya taifa ya Marekani kuichapa Serbia ya Nikola Jokic kwa pointi 95-91 baada ya Serbia kuongoza kwa muda mrefu mchezo huo mkali.

WAKATI jana Jumamosi usiku mastaa wa ligi ya kikapu ya NBA, Lebron James na Steph Curry walikuwa kwenye msako wa medali ya dhahabu ya Olimpiki katika mchezo wa fainali dhidi ya wenyeji Ufaransa, ratiba mpya ya msimu ujao imeshatoka na kubwa zaidi ni ile ya siku ya Krismasi ambayo imeshiba mechi tano kali.

LeBron, Kevin Durant na Curry kwa pamoja ndio walichangia ushindi mgumu wa timu yao ya taifa ya Marekani kuichapa Serbia ya Nikola Jokic kwa pointi 95-91 baada ya Serbia kuongoza kwa muda mrefu mchezo huo mkali.

Curry alifunga pointi 36 zikiwa ni nyingi zaidi kwenye Olimpiki kwa mchezaji wa taifa hilo, huku LeBron akifunga triple-double nyingine na kuandikisha rekodi hiyo kwenye Olimpiki zaidi ya moja huku KD akishikilia rekodi ya muda wote kwa Marekani kuwa na pointi nyingi zaidi.

Mastaa hao kwenye NBA msimu ujao wanasubiriwa kuzibeba timu zao.


CURRY VS LEBRON

Huu ni mchezo ambao mara zote huvuta hisia kwa wapenzi wa NBA duniani kutokana na kuwakutanisha mastaa wawili wakubwa Steph Curry na LeBron James ambao vita yao ilianzia wakati LeBron akiwa Cleveland Cavaliers na baadaye Los Angeles Lakers aliyopo hivi sasa.

Siku hiyo ya Krismasi, LeBron na Curry watakuwa kwenye vita ya kuongoza timu mojawapo kati ya Lakers au Warriors kuibuka na ushindi ambao haukwepeki, Warriors watakuwa nyumbani uwanjani Chase Center.

Mchezo huo utakuwa ni mwendelezo wa shoo kali baina ya mastaa hao ambao wamevuta hisia kwa kucheza kwa pamoja kwa mara ya mwisho kwenye Olimpiki ya Ufaransa inayomalizika leo.


KD VS MVP JOKIC

Vita ya MVP wa NBA msimu uliopita, Nikola Jokic ilikuwa kubwa dhidi ya mastaa watatu Curry, LeBron na KD kwenye nusu fainali ya Olimpiki Alhamisi, vita baina ya mmojawapo ambaye ni Durant itajirudia tena siku ya Krismasi pale Phoenix Suns itakapoikaribisha Denver Nuggets ya Jokic, Jamal Murray na Russell Westbrook.

Mbali na KD, Suns ina wakali wengine Devin Booker na Bradley Beal ambao wanatengeneza utatu mkali unaotisha na bado unasubiriwa kufanya kitu ikiwamo kushinda taji la NBA baada ya timu hiyo kucheza fainali mwaka 2021 dhidi ya Milwaukee Bucks.


EMBIID VS TATUM

Mchezo mwingine mkali siku hiyo ni ule baina ya bingwa mtetezi, Boston Celtics kuwakaribisha Philadelphia 7ers ambayo inaongozwa na Joel Embiid wakati Celtics inaongozwa na Jayson Tatum waliocheza pamoja kwenye kikosi cha Marekani katika Michezo ya Olimpiki.

Utamu wa mchezo huo unatokana na timu hizo kuwa kwenye vita ya kusaka ubingwa wa Mashariki kwa miaka ya hivi karibuni, kabla ya Celtics kufanikiwa kushinda vita hiyo na sasa ni mabingwa watetezi wa taji la NBA.


ANT MAN KULIPA KISASI?

BAADA ya Anthony Edwards kuiongoza Minnesota Timberwolves kuwavua taji Denver Nuggets kwenye nusu fainali ya ukanda wa Magharibi, walitarajiwa kucheza fainali ya jumla dhidi ya bingwa wa Mashariki, lakini haikua hivyo walipokwama mbele ya Dallas Mavericks ya Luka Doncic na Kyrie Irving.

Timberwolves sasa wamepewa Dallas kwenye siku ya Krismasi ili wajiulize upya kama watalipiza kisasi.


WEMBANYAMA VS BRUNSON

Staa wa Ufaransa, Victor Wembanyama ameliongoza taifa hilo kucheza fainali ya Olimpiki 2024 kwa kuzitoa timu ngumu ikiwemo Ujerumani ambao ni mabingwa wa dunia na kabla ya hapo robo fainali waliitoa nishai Canada iliyopewa nafasi kubwa kucheza fainali dhidi ya ndugu zao Marekani.

Siku hiyo ya Krismasi, Wembanyama akiwa na mkongwe Chris Paul watakuwa na kazi pevu ugenini mbele ya New York Knicks ya Jalen Brunson na Mikal Bridges na mastaa wengine wanaoifanya timu hiyo iwe kwenye nafasi ya timu zinazopewa nafasi kubwa kushinda taji.