Kazini kwa Alexander-Arnold kuna kazi!

Muktasari:
- Hilo ni kwa mujibu wa mtaalamu wa soka la Hispania, Terry Gibson, ambaye ametia shaka kubwa kwa Trent juu ya kuwa na uhakika wa kucheza beki wa kulia huko Los Blancos.
MADRID HISPANIA: BEKI, Trent Alexander-Arnold ameambiwa asijidanganye kwamba amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha Real Madrid kwa sababu anayecheza nafasi hiyo ni mbishi.
Hilo ni kwa mujibu wa mtaalamu wa soka la Hispania, Terry Gibson, ambaye ametia shaka kubwa kwa Trent juu ya kuwa na uhakika wa kucheza beki wa kulia huko Los Blancos.
Alexander-Arnold aliondoka Liverpool kwenda kujiunga na Madrid baada ya mkataba wake huko Anfield kufika ukomo mwishoni mwa msimu uliopita.
Alijiunga na Real Madrid mapema na kwamba miamba hiyo ya Hispania ililazimika kuilipa Liverpool ili tu kumpata mchezaji huyo akaungane na kikosi chao kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
Na tangu wakati huo amekuwa panga pangua anaanza kwenye kikosi hicho chini ya kocha Xabi Alonso, ambapo alianzishwa kwenye kila mechi ambayo timu yake imecheza kwenye fainali hizo za Marekani.
Licha ya kwamba Alexander-Arnold, mwenye jezi Namba 12, amekuwa akianza kwa sasa kwenye beki ya kulia, hilo linaweza kubadilika muda wowote kutokana na mchezaji mwingine anayecheza hapo.
Gwiji wa Real Madrid, Dani Carvajal ni mbishi na atakwenda kumpa Trent upinzani mkali sana kwenye nafasi ya kuanza katika beki hiyo ya kulia.
Carvajal, ambaye ameshinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni moja ya wachezaji wa Los Blancos wenye uzoefu mkubwa, akicheza zaidi ya mechi 400 kwa zaidi ya miaka 12 aliyokuwa hapo.
Ndiyo kwanza anarejea kwenye utimamu wake baada ya kusumbuliwa na maumivu ya goti Oktoba mwaka jana na bila shaka kurejea kwake kikosini, atahitaji kuanza msimu ujao.
Na sasa mtaalamu huyo wa soka la Hispania, Gibson anaamini itakuwa utata mkubwa kufanya uamuzi wa kumwanzisha Alexander-Arnold mbele Carvajal.
Gibson alisema: “Ndiyo, asilimia 100, Trent nafasi yake ya kuanza haina uhakika. Naweza kusema kwamba Dani Carvajal bado ana nafasi kubwa. Ni gwiji na kwa mataji yote ya Ligi ya Mabingwa Ulaya aliyobeba, amefanya hivyo kwa moyo mkubwa kwenye kikosi cha Madrid. Itakuwa utata mkubwa kwa Xabi Alonso kumweka kando.”
Gibson aliongeza: “Itashangaza asipomtumia Carvajal, lakini itategemea na namna atakavyorejea uwanjani akitokea kwenye maumivu ya goti. Pengine hatutaona ubora wake sasa hadi hapo Krismasi. Lakini, kutakuwa na ushindani mkali, kwa sababu Carvajal ni beki mzuri. Alexander-Arnold naye hakuna ubishi, ni mzuri na zile pasi zake. Wawili hao, wapo tofauti uchezaji wao.
“Ninachokiona Carvajal ana nafasi kubwa kwa sababu ni mzuri katika kila kitu. Alexander-Arnold ni mzuri kwenye jambo moja au mawili, hayupo vizuri kwenye ulinzi.”
Staa huyo wa zamani wa Liverpool mara kwa mara amekuwa akikosolewa kutokana na kuonyesha udhaifu mkubwa kwenye kukaba, ambalo hilo ni eneo la ubora wa Carvajal, huku kibarua kinachomkabili kocha Alonso ni kuhakikisha anawaweka fiti mastaa wote hao wawili.
Kwa maana hiyo ni rahisi kusema kazini kwa Trent na Carvajal kuna kazi. Real Madrid itakipiga na Borussia Dortmund kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu.
Lakini, mechi yao ya kwanza kwenye LaLiga wakati wa msimu mpya watakabiliana na Osasuna, Agosti mwaka huu na hapo ndipo kitaeleweka nani ni nani kwenye beki ya kulia ya Real Madrid.