Kasi La Liga kiboko

Ligi ya Hispania 'La Liga' imeweka rekodi ya kuongoza kwa wachezaji wake kukimbia umbali mrefu ndani ya uwanja kulinganisha na ligi nyingine duniani

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya utafiti wa masuala ya mpira wa miguu ya CIES kwa ligi 31 duniani umefichua kwamba katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu ya Hispania, wachezaji wanakimbia wastani wa jumla umbali wa Kilomita 103.7

Ligi hiyo ya Hispania inafuatiwa kwa ukaribu na Ligi Kui ya Sweden ambayo kwa mchezo mmoja, wachezaji wanakimbia wastani wa kilomita 103.6 wakati Ligi Kuu ya Uholanzi iko nafasi ya tatu kwa umbali wa wastani wa kilomita 103.5 ambao wachezaji wake wanakimbia kwa mchezo mmoja.

Ligi ya Italia na Poland, ziko katika nafasi ya nne na ya tano katika chati hiyo ambapo wastani wa kilomita ambazo wachezaji wanakimbia kwa mchezo kwenye kila ligi ni kilomita 102.8.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kati ya kundi la Ligi 31 zilizohusishwa, Ligi Kuu ya Brazil ndio ligi ambayo wachezaji wake wanakimbia kilomita chache zaidi ndani ya uwanja  kwa wastani

Wastani wa kilomita ambazo wachezaji wanakimbia kwa mchezo kwenye Ligi Kuu ya Brazil ni 95.8

Utafiti huo umeonyesha kuwa  Ligi ya England inashika nafasi ya 11 ambapo wachezaji kwa mchezo wanakimbia wastani wa Kilomita 100.8 kwa mechi wakati Ligi ya Mabingwa Ulaya iko nafasi ya saba kwa wastani wa kilomita 101.9 ambao wachezaji wanakimbia kwa mechi.