Kaka wa Pogba atupwa jela Ufaransa

Muktasari:
- Mathias Pogba pamoja na watu wengine watano walifikishwa mahakamani mwaka 2022, wakishitakiwa kwa njama za ulaghai na uhalifu ambao walikuwa wakimfanyia Pogba.
PARIS, UFARANSA: Kaka yake Paul Pogba anayejulikana kwa jina la Mathias Pogba, amehukumiwa kwenda jela kwa miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kutaka kumteka na kumlaghai kiungo huyo wa zamani wa Manchester United.
Mathias Pogba pamoja na watu wengine watano walifikishwa mahakamani mwaka 2022, wakishitakiwa kwa njama za ulaghai na uhalifu ambao walikuwa wakimfanyia Pogba.
Taarifa zinasema kuwa watuhumiwa hao walimdai Pogba dola 14.3 milioni wakimtishia kuwa watafichua baadhi ya siri zake pia wakimtishia mara kwa mara, kundi hilo linatuhumiwa kwa kufanya vurugu, utekaji nyara, na kumfunga Pogba ili kuwezesha ulaghai huo na wakati wa uchunguzi, Pogba alikiri kulipa dola 70,000 kwa kundi hilo akiwemo kaka yake.
Kesi hiyo ilijulikana hadharani mwezi Agosti 2022, baada ya Mathias kuposti video kwenye mitandao ya kijamii, akidai kuwa angefichua taarifa za kushtua kuhusu kaka yake Paul.
"Kutokana na hayo, njia pekee ya kujinusuru ambayo mimi [Mathias] ninayo ni kufichua uongo wake [Paul] na udanganyifu wake.
“Ndiyo maana nilithibitisha uchawi wake kwa sababu cha muhimu hapa si kwamba uniamini au usiniamini, ni kwamba ina nia mbaya kwa sababu uchawi huu unategemea kufanya mambo mabaya kwa matambiko na anamfanyia pia mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe," alisema Mathias akizungumza na Get French Football News.
Mathias alikamatwa muda mfupi baadaye na kufunguliwa kesi kwenye Mahakama ya Paris ambayo hukumu iliyotoka leo imempeleka gerezani kwa miaka mitatu, lakini wakili wake ameshasema kuwa watakata rufaa kuhusu hukumu hiyo kwa kuwa anaamini mteja wake hana hatia.
Kwa mujibu wa Pogba, kaka yake alitumia mbinu nyingi kuhakikisha kuwa anawapa fedha kiasi chochote walichokuwa wanataka.