Liverpool yadhamiria kwa Alexander Isak, kuvunja rekodi

Muktasari:
- Isak mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akiwindwa na vigogo wa Ulaya tangu msimu uliopita lakini changamoto kubwa ni ada ya uhamisho ambayo Newcastle inaihitaji ili kumuuza.
LIVERPOOL iko tayari kuvunja rekodi ya usajili England ili kuinasa saini ya mshambuliaji wa Newcastle na timu ya taifa ya Sweden, Alexander Isak, katika dirisha hili.
Isak mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akiwindwa na vigogo wa Ulaya tangu msimu uliopita lakini changamoto kubwa ni ada ya uhamisho ambayo Newcastle inaihitaji ili kumuuza.
Kwa mujibu wa ripoti, mabosi wa Newcastle wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 150 milioni na licha ya baadhi ya timu kufanya nao mazungumzo ili kukipunguza, vigogo hao wanadaiwa kukataa.
Hakuna uhakika wa asilimia mia ikiwa Liverpool italipa kiasi chote cha Pauni 150 milioni lakini inaaminika kuwa wamepanga kulipa kiasi kinachokaribia na dau hilo.
Kocha wa majogoo hawa wa Jiji la Liverpool, Arne Slot inadaiwa ni shabiki mkubwa Isak na anaamini ikiwa atatua katika kikosi atasaidia sana kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Liverpool inataka kuimarisha kikosi chake ili kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao na inatarajiwa kuachana na baadhi ya nyota wake na kushusha wengine wa maana.
Patrik Schick
ARSENAL ipo katika vita kali dhidi ya timu za Seria A ya kuipata huduma ya mshambuliaji wa Bayer Leverkusen na Jamhuri ya Czech, Patrik Schick, 29, dirisha hili. Ripoti kutoka tovuti ya Skysports zinadai Leverkusen haitaki kumuuza staa huyo kwa sasa kwani inaona itakuwa inaivunja timu yao kwa kuwa kuna kundi kubwa la wachezaji tayari washaondoka lakini wanaweza kuamua kumuuza ikiwa itapatikana ofa nono.
Nick Pope
KIPA wa Newcastle United raia wa England, Nick Pope, mwenye miaka 33, hataki kuondoka Newcastle licha ya Leeds kuonyesha nia ya kutaka kumsajili dirisha hili la majira ya kiangazi. Inaelezwa Pope hajavutiwa na ofa ya Leeds licha Newcastle kuwa tayari kumuuza kwenda timu hiyo. Mkataba wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Yoane Wissa
BRENTFORD inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni kutoka kwa timu yoyote itakayohitaji saini ya mshambuliaji wao raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Yoane Wissa, katika dirisha huli. Staa huyu anawindwa na timu kibao ndani na nje ya bara la Ulaya ikiwa pamoja na Nottingham Forest, Tottenham, Arsenal, Fenerbahce na Galatasaray.
Joao Pedro
CHELSEA imewasiliana na Brighton kuhusu mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Joao Pedro, mwenye miaka 23, ambaye pia anawaniwa na Newcastle. Pedro ambaye msimu uliopita alicheza mechi 30 za michuano yote na kufunga mabao 10, ameziingiza vitani timu nyingi katika dirisha hili baada ya Brighton kudaiwa kuwa tayari kumuuza ikiwa itapokea ofa nono.
Emi Buendia
ASTON Villa iko tayari kumuuza kiungo wao Emi Buendia, mwenye umri wa miaka 28, iwapo watapokea ofa ya zaidi ya kuanzia Pauni 20 milioni au zaidi kwa ajili ya staa huyo. Buendia mwenye umri wa miaka 28, anadaiwa kuwa mmoja kati ya mastaa ambao hawapo katika mipango ya Unai Emery kwa msimu ujao kiasi cha kocha huyo kutoa ruhusa auzwe.
Morgan Rogers
CHELSEA bado ina mpango wa kumsajili kiungo wa Aston Villa na England, Morgan Rogers, mwenye miaka 22, ikiwa Aston Villa itakuwa tayari kumuuza dirisha hili. Rogers ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Villa, mkataba wake wa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030, msimu uliopita alicheza mechi 54 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Myles Lewis-Skelly
BEKI wa pembeni wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly, 18, yuko karibu kusaini mkataba mpya utakaomfanya kuwa mmoja wa wachezaji chipukizi wanaolipwa vizuri zaidi duniani. Vigogo wa Arsenal wanataka kumpa Myles mkataba huo mnono baada ya hivi karibuni Real Madrid kudaiwa kuanza kumnyemelea. Msimu uliopita alionyesha kiwango bora na kuifanya Arsenal kumaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Liverpool na sasa anapewa mkataba mnono ili azidi kuwa na makali.