Trent atoa siri ya Kihispania chake

Muktasari:
- Nyota huyo wa kimataifa wa England aliwaacha mashabiki wa zamani wa Liverpool midomo wazi alipohutubia familia, marafiki na wanahabari kwa Kihispania fasaha wakati wa utambulisho wake rasmi kama mchezaji wa Madrid wiki iliyopita.
FLORIDA, MAREKANI: BEKI kisiki wa Real Madrid, Trent Alexander-Arnold amefichua alikuwa akijifunza Kihispania kwa ‘miezi kadhaa’ kabla hajajiunga na timu hiyo dirisha hili.
Nyota huyo wa kimataifa wa England aliwaacha mashabiki wa zamani wa Liverpool midomo wazi alipohutubia familia, marafiki na wanahabari kwa Kihispania fasaha wakati wa utambulisho wake rasmi kama mchezaji wa Madrid wiki iliyopita.
Baada ya mechi yake ya kwanza ambayo haikuwa rahisi akiwa na Madrid, beki huyo wa kulia aliulizwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu uwezo wake wa kuzungumza Kihispania na alikiri alijifunza lugha hiyo kwa miezi kadhaa kabla ya uhamisho wake.
Akizungumza na DAZN alisema:
“Nimekuwa nikijifunza Kihispania kwa miezi michache. Nilipogundua nitahamia Madrid, nilitaka nijifunze ili niweze kuzoea mazingira.”
“Nchi mpya, timu mpya, na jiji jipya. Ni muhimu kuonyesha unahitaji kuzoea utamaduni. Hilo ndilo nililokuwa nafanya.”
Wadau wengi wa soka walishangazwa na uwezo wake wa kuzungumza Kihispania kwa sababu waliamini kwa kuwa ameitumikia Liverpool tu katika maisha yake yote ya soka asingekuwa anafahamu kabisa lugha hiyo.
Hata hivyo, wengi walishangazwa alipotoa hotuba nzima kwa Kihispania, na kufichua kwamba kujiunga na mabingwa wa Ulaya mara 15 ni “ndoto iliyotimia.”
Baadhi ya mashabiki wa Liverpool, pamoja na mashabiki wa soka kwa jumla, walijiuliza Alexander-Arnold amewezaje kuimudu lugha hiyo kwa haraka.
Mashabiki wengine waliweka wazi huenda Alexander-Arnold alikuwa ameanza kupanga kuondoka Liverpool muda mrefu zaidi kuliko ilivyodhaniwa.
Mmoja aliandika: “Huyu jamaa amekuwa akipanga uhamisho huu kwa muda mrefu.”
Mwingine alikubaliana: “Bila shaka Trent alijiandaa na kupanga uhamisho wake kwa karibu miaka miwili.”