Jamie Carragher: Salah huyu mbona wetu
Muktasari:
- Salah amekuwa mmoja wa wachezaji nyota kwenye kikosi cha Arne Slot msimu huu, lakini bado kuna uwezekano wa kuondoka wakati mkataba wake utakapomalizika.
LIVERPOOL, ENGLAND: LEJENDI wa Liverpool, Jamie Carragher ametaja sababu inayomfanya aamini kuwa Mohamed Salah ataongeza mkataba wa kuendelea kusalia Liverpool baada ya msimu huu kumalizika.
Salah amekuwa mmoja wa wachezaji nyota kwenye kikosi cha Arne Slot msimu huu, lakini bado kuna uwezekano wa kuondoka wakati mkataba wake utakapomalizika.
Tovuti ya Daily Mail Sport iliripoti wiki iliyopita kuwa licha ya timu kumpa ofa ya mkataba mpya Salah bado kuna mjadala kuhusu masuala ya malipo ambao ndio unakwamisha Salah kusaini.
Salah alikuwa amewaambia waandishi wa habari baada ya ushindi wa 3-2 wa Liverpool dhidi ya Southampton kuwa nafasi yake ya kubaki ni “ndogo”.
Hata hivyo, Carragher anaendelea kuwa na matumaini kwamba Salah atasalia katika klabu yake hiyo.
“Ni mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea Liverpool, nampenda Mo Salah, ni mmoja wa wachezaji bora duniani, lakini naamini atabaki kwa sababu ya umri wake. Unapokuwa na umri kama wake na hali aliyonayo ili kuondoka anahitaji kupata timu itakayokuwa tayari kumpa zaidi na sio ongezeko la Pauni 10,000 au 20,000, hapana ni zaidi ya hapo.”
Carragher aliongeza kuwa nafasi za Salah kuhamia timu kubwa za Ulaya kama Real Madrid au Barcelona ni ndogo kutokana na changamoto za kifedha za klabu hizo na hata viwango vyao katika michuano mbalimbali.
“Ni timu chache tu, labda nne au tano, ambazo zinaweza kushinda Ligi ya Mabingwa, na Liverpool ni mojawapo.”