Henry: Guardiola? Anachopitia nakijua

Muktasari:
- Mambo yamekwenda kombo kwa Guardiola katika mambo ya nje ya uwanja, huku ndani ya uwanja nako shughuli ni pevu na kikosi chake cha Man City kukumbana na kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Arsenal kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Jumapili iliyopita.
MANCHESTER, ENGLAND: THIERRY Henry amesema Pep Guardiola hayupo sawa baada ya kocha huyo wa Manchester City kuachana na mkewe, mrembo Cristina Serra.
Mambo yamekwenda kombo kwa Guardiola katika mambo ya nje ya uwanja, huku ndani ya uwanja nako shughuli ni pevu na kikosi chake cha Man City kukumbana na kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Arsenal kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Jumapili iliyopita.
Man City itahitaji kucheza mechi ya mchujo kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwenda Ligi Kuu England imeachwa kwa pointi 12 na vinara Liverpool baada ya kushinda mechi nne tu kati ya 10 zilizopita kwenye ligi hiyo.
Guardiola, 54, alifichua mwezi uliopita ameachana na mkewe, ambaye alidumu naye kwenye ndoa kwa miaka 36.
Henry, ambaye alicheza chini ya Guardiola alipokuwa Barcelona, ameonyesha huruma yake kwa bosi wake huyo wa zamani baada ya kipigo cha Arsenal.
Alisema: “Naona huruma kinachotokea Man City na Pep? Ndiyo, naona huruma. Sio kitu rahisi kukabiliana na yanayomkabili Pep nje ya uwanja.
"Nilipita hizo nyakati wakati nilipokwenda Barcelona. Sio kitu rahisi kukabiliana na mambo hayo, hasa unapokuwa haupo sawa kiakili. Unaweza kuona kabisa, Pep sio yeye kabisa. Mimi nilikabiliana na hali hiyo nilipokwenda Barcelona, niwaambie sio kitu rahisi.
"Hakuna mtu anaweza kukabiliana na mambo kama hayo kisha akafanya vizuri muda wote. Nadhani tunapaswa kuelewa hilo.”
Henry, 47, aliachana na mkewe, mrembo Claire Merry mwaka 2007 baada ya kuwa kwenye ndoa kwa miaka minne. Mrembo alihitaji apewe mgawo wa Pauni 10 milioni kwenye kuachana kwao na Henry. Kuhusu Guardiola na mrembo Cristina walikutana wakiwa wadogo kabisa na kufanikwa kupata watoto watatu, Maria, 24, Marius 22, na Valentina, 17.