Guardiola ajibebesha lawama 

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amejibebesha lawama nyingi baada ya kuzidiwa pointi nane na vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal kuelekea kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa msimu huuu.

Man City ilipoteza michezo miwili katika mechi tano za Ligi Kuu England ilizocheza huku kocha huyo akisisitiza ana kazi kubwa kuhakikisha vijana wake wanarejea mchezoni akiwemo straika wa timu hiyo Erling Haaland.

Haaland hajacheka na nyavu katika mechi tatu za mwisho alizocheza ikiwa ni rekodi mbovu aliyoweka kwa mara ya kwanza tangu anatua Etihad kwa kitita cha Pauni 51 milioni akitokea Borussia Dortmund.

Akizungumza na waandishi habari, Guardiola amesema yeye ndiye chanzo kama timu haionyeshi kiwango kizuri kwenye mechi kwa hiyo anastahili kubeba lawama zote.

"Mimi ndiye mhusika mkuu kwenye hili, natakiwa nitafute njia mbadala, hii ni kazi yangu, lazima nijiongeze kuhakisha timu inapata matokeo mazuri, kila mtu anajiuliza kwa nini imetokea hivi? Kwa nini Man City haiongozi ligi, hili ni jukumu langu natakiwa niwepo na kuiongoza timu katika mashindano yote," alisema Guardiola.

Guardiola alijawa na hofu kutokana na mwenendo wa kikosi chake lakini amewaomba wachezaji wake watulize mzuka kwa sababu anaamini ni kipindi cha mpito.
Hivi karibuni Guardiola aligeuka kuwa mbogo na kukiri Haaland hapewi ushirikiano ili aendane na mfumo kwani anasahaulika sana.

Haaland alipata nafasi chache kwenye mechi ya Manchester Derby uliyochezwa wiki iliyopita, Man City ikipokea kichapo cha mabao 2-1. Hadi mpira unamalizika Haaland aligusa mipira mara 19 tu.

Nyota huyo wa kimataifa wa Norway amefunga mabao 27 katika mechi 21 alizocheza lakini Guardiola hakupendezwa na namna Haaland alivyokuwa akipata ugumu katika mechi za tatu za mwisho alizocheza.

"Ngumu sana Haaland hapati mipira ya mwisho iliyokuwa sahihi, atafutiwe nafasi zaidi, aligusa mipira mara chache sana dhidi ya Man United, alikuwa kama wamemsahau hivi, kuna maeneo wanapaswa kutambua, Haaland ni mfungaji mzuri lakini mambo kama haya yanatakiwa kuzingatiwa," alisema Guardiola.