Greenwood, Donny van de Beek kuinufaisha Man United

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa dirisha hili taarifa zimekuwa zikidai kwamba Man United ipo tayari kuuza kundi kubwa la wachezaji ambao hawapo katika mipango ya timu kwa msimu ujao ili kusuka upya kikosi kwa kusajili mastaa kutokana na pesa itakazopata.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United ipo karibu kuuza nyota wake Mason Greenwood, Donny van de Beek katika dirisha hili la usajili ikiwa ni sehemu ya mpango kutafuta pesa itakazotumia kufanya usajili wa wachezaji wapya baada ya bajeti kubana.

Tangu kuanza kwa dirisha hili taarifa zimekuwa zikidai kwamba Man United ipo tayari kuuza kundi kubwa la wachezaji ambao hawapo katika mipango ya timu kwa msimu ujao ili kusuka upya kikosi kwa kusajili mastaa kutokana na pesa itakazopata.

Mashetani Wekundu wameingia katika dirisha hili wakiwa na bajeti ya Pauni 50 milioni ambazo ndizo watatakiwa kuzitumia kufanya usajili, lakini mpango wa viongozi ni kuongeza pesa kwa kuuza wachezaji.

Hadi sasa, mbali ya kuwa katika hatua nzuri ya kumsajili straika wa Bologna, Joshua Zirkzee ambaye anauzwa kwa Pauni 34 milioni, Man United pia inahitaji beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.

Tovuti ya Mirror Football  inaeleza kwamba Man United inatarajiwa kuingiza kati ya Pauni 30 hadi 35 milioni kwa mauzo ya Greenwood ambaye ameshafikia makubaliano ya kujiunga na Marseille ya Ufaransa ikiwa ni siku mbili tangu alipokutana na viongozi wa juu wa Man United kujadili hatma yake.

Vilevile Mirror imeripoti kwamba Van de Beek ambaye alijiunga kwa ada ya Pauni 35 milioni akitokea Ajax mwaka 2020 naye anaondoka kwa mkopo kujiunga na Girona katika dili ambalo Man United itapata Pauni 450,000 kama ada ya uhamisho wa mkopo na ndani ya mkataba kuna kipengele kinachoeleza kwamba ikiwa itavutiwa na kiwango chake kiasi cha kutaka kumsajili itatakiwa kulipa Pauni 16 milioni.

Staa mwingine anayekaribia kuondoka ni Sancho, ingawa hadi sasa hakuna timu iliyoripotiwa kuwasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili ingawa taarifa zinadai timu kibao kutoka Italia kama Juventus zimeonyesha nia ya kutaka kuwasilisha ofa ili kumpata.

Hata hivyo, Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Borussia Dortmund anaweza kubaki ikiwa ataomba msamaha kwa kocha Erik ten Hag, lakini uwezekano huo hauonekani kuwapo hadi sasa.

Man United ipo tayari kumwachia nyota huyo ikiwa timu yoyote inayomtaka italipa Pauni 40 milioni kiasi ambacho kinazirudisha timu nyingi nyuma kwani zinaamini ni kikubwa.

Mastaa wengine wanaouzwa ni wale wanaowindwa na timu za Uturuki ikiwa pamoja na Victor Lindelof anayehitajika na  Fenerbahce sambamba na Aaron Wan-Bissaka aliye katika rada za Galatasaray na West Ham United.

Facundo Pellistri anaweza kurudishwa Hispania ambako msimu uliopita alicheza kwa mkopo Granada na sasa Real Valladolid inadaiwa kuitaka huduma yake. Kiungo wa Kibrazili, Casemiro yupo mbioni kuuzwa Saudi Arabia na mbali ya kupata pesa itakazomuuzia, pia Man United itapunguza bajeti ya kulipa mishahara kwani Mbrazili huyo anakunja  Pauni 375,000 kwa wiki.

Mchezaji mwingine ni Scott McTominay anayemezewa mate na Fulham pamoja na Everton, na moja ya timu hizo imewasilisha ofa ya Pauni 30 milioni ikakataliwa na Man United inayohitaji zaidi ya hiyo.