Everton yaikomalia Man United kwa  Branthwaite

Everton Pict
Everton Pict

Muktasari:

Man United imewasilisha ofa hiyo ya Pauni 45 milioni sambamba na ongezeko la Pauni 5 milioni ili kumpata Jarrad ambaye imekuwa ikiiwania saini yake tangu dirisha la usajili lifunguliwe.

LIVERPOOL, ENGLAND: EVERTON imekataa ofa ya pili ya Manchester United ya Pauni 50 milioni kwa ajili ya kumuuza beki wao Jarrad Branthwaite.

Man United imewasilisha ofa hiyo ya Pauni 45 milioni sambamba na ongezeko la Pauni 5 milioni ili kumpata Jarrad ambaye imekuwa ikiiwania saini yake tangu dirisha la usajili lifunguliwe.

Mbali ya ofa hiyo, mashetani hawa wekundu wapo tayari kumpa Jarrad mwenye umri wa miaka 22, mshahara unaofikia Pauni 160,000 kwa wiki.

Kwa mujibu wa ripoti, Everton imeendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji Pauni 70 milioni ili kumuuza beki huyo jambo litakaloilazimisha Man United kuwasilisha ofa nyingine ya tatu.

Taarifa kutoka tovuti ya Daily Mail zinaeleza mabosi wa Man United walikuwa na kikao kizito Jumatatu ya wiki hii kujadili ikiwa watatuma ofa nyingine mpya kwenda Everton kwa ajili ya Jarrad au laa.

Baada ya majadiliano katika kikao hicho wakakubaliana watatuma ofa kwa ajili ya Jarrad lakini bahati mbaya kwao imekataliwa tena.

Mbali ya kujadili kuhusu beki huyo, Man United pia ilijadili kuhusu straika wa Bologna Joshua Zirkzee na walifika mwafaka wa kuwasilisha Pauni 34 milioni kwa ajili ya kuvunja mkataba wake.

Mbali ya Jarrad, Man United pia inahitaji huduma ya beki wa Bayern Munich, Matthijs de Ligt.