Eti nini? Haaland, Barca ni Pauni 1 bilioni

BARCELONA, HISPANIA. WAKALA wa straika wa Manchester City Erling Haaland ameeleza kuwa hatoweza kukataa ikiwa Barcelona itakuja mezani na kuhitaji huduma ya staa huyo ingawa inaweza kuwagharimu zaidi ya Pauni 1 bilioni au zaidi kama ada ya usajili.

Haaland mwenye umri wa miaka 22, kwa sasa ni mmoja kati ya wachezaji bora kwenye EPL akiwa na Man City aliyojiunga nayo katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi akitokea  Borussia Dortmund.

Msimu huu tayari ameshafunga mabao 31 kwenye mechi 27 za michuano yote alizocheza akiwa ndio mfungaji kinara wa Ligi Kuu England hadi sasa.
Wakala wake kwa sasa ambaye ni Rafaela Pimenta aliyeachiwa madaraka na Mino Raiola wakati alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti la Hispania la AS, alieleza kuwa itakuwa ni ngumu sana kwake kusema hapana kwa rais wa Barcelona ikiwa atasema anamtaka Haaland kutokana na ukaribu ambao rais huyo Joan Laporta alikuwa nao Mino.

“Kila siku nimekuwa nikisema, Laporta hawezi kuniomba chochote kinachohusiana na mpira wa miguu kwa sababu anajua akiniambia nitasema ndio,''alisema Pimenta alipoulizwa ikiwa atakubali ofa ya Barca pindi watakapomhitaji Haaland.
Haya hivyo wakala huyo mrembo aliongeza kwa sasa Haaland ni mchezaji wa Man City na mkataba wake utamalizika mwaka 2027, hivyo wenye uamuzi wa mwisho kabisa itakuwa mabosi wa timu hiyo ikiwa watataka kumuuza au la.

Vilevile akataja kwamba thamani ya staa huyo inazidi kuongezeka siku hadi siku na mbali ya ada ya uhamisho kuna masuala mengine kama haki za matangazo ya picha na udhamini  ambapo kwa pamoja zinamfanya fundi huyo kuwa na thamani ya zaidi ya Pauni 1 bilioni.

“Nafahamu kwamba hakuna timu inayoweza kulipa Pauni 700 milioni kwa ajili ya kununua mchezaji, lakini nina uhakika wa asilimia kwamba thamani ya Haaland kwa sasa ikiwa timu yoyote itamhitaji ni zaidi ya Pauni 1000 milioni(Pauni 1 bilioni).
Kabla ya kutua Manchester City, Haaland alikuwa akiwindwa na timu nyingi barani Ulaya ikiwa pamoja na Barcelona lakini mahitaji yake yalikuwa makubwa sana kwa vigogo hao na wakaamua kuachana naye.

Fundi huyu alitua kwenye kikosi cha Man City kwa ada ya  uhamisho ya Euro 60 milioni ambayo ilikuwa ni bei iliyowekwa kwenye mkataba wake lakini mshahara anaokunja kwa wiki unafikia Pauni 800,000 ikiwa pamoja na mjumuisho wa bonasi na kiasi hicho kimemfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi nchini England.

Kabla ya kupoteza maisha Raiola alimuachia majukumu yote Pimenta ambapo kwa sasa yeye ndio anawasimamia mastaa kama Paul Pogba, Romelu Lukaku na Gianluig Donnarumma waliokuwa wakisimamiwa na Mino kabla ya kupotea maisha.
Alikuwa akifanya kazi na Raiola kwa miaka 18 ambapo alihudumu kama mwanasheria wake maalumu kwa ajili ya masuala ya kesi za wachezaji wake.