EL CHOLO: Hana njaa, Sh330 bilioni imetulia benki

Muktasari:
- Au ndo pesa yako unaweka kwenye simu? Sawa, salio lako linasomaje? Usipate hasira, maisha ndivyo yalivyo. Hayajawahi kutenda haki.
MADRID, HISPANIA: VIPI, hivi una akaunti ya benki? Na kama unayo, salio linasomaje huko?
Au ndo pesa yako unaweka kwenye simu? Sawa, salio lako linasomaje? Usipate hasira, maisha ndivyo yalivyo. Hayajawahi kutenda haki.
Wakati wewe ukijikuna kichwa kutaja salio lako la pesa, kuna mtu kwenye akaunti yake ya benki salio lake ana mabilioni ya shilingi.
Unamjua El Cholo? Usipasuke kichwa kumuwaza ni nani. Ni huyu, Diego Pablo Simeone Gonzalez. Mara nyingi, umekutana na jina lake likiandikwa, Diego Simeone. Kwa mashabiki wa soka, wamemshapata. Ndiye kocha wa timu ya soka ya Atletico Madrid inayoshiriki ligi ya La Liga, Hispania.
Kinachoripotiwa ni pato la El Cholo ni Dola 130 milioni, kwa mkwanja wa Kitanzania ni Sh331 bilioni.

Kwani El Cholo ni nani?
Wakati anazaliwa Aprili 28, 1970 wazazi wake walimpa jina la Diego Pablo Simeone Gonzalez. Ni kocha wa mchezo wa soka na staa wa zamani wa mchezo huo aliyetamba kwenye safu ya kiungo. Amekuwa Kocha wa Atletico Madrid, tangu Desemba 23, 2011.
Maisha yake ya kuchezea soka la klabu yalianzia mwaka 1987. Simeone alicheza soka Argentina, Italia na Hispania kwenye klabu za Velez Sarsfield, Pisa, Sevilla, Atletico Madrid, Inter Milan, Lazio na Racing Club. Alishinda mataji ya kutosha katika timu hizo.

Kwenye ukocha, Simeone amezinoa klabu za Racing Club, Estudiantes, River Plate, San Lorenzo na Catania, kabla ya kujiunga na Atletico mwaka 2011. Mafanikio yake makubwa kwenye ukocha alipata akiwa na Atletico na amebeba ubingwa wa La Liga mbele ya vigogo Real Madrid na Barcelona. Tena amefanya hivyo mara mbili, huku akibeba Europa League mara mbili, Uefa Super Cup mara mbili na amecheza mara mbili fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na zote alipoteza mbele ya mahasimu wake wa Jiji la Madrid, Real Madrid.

Pesa ametoa wapi?
Kazi kubwa ya Simeone ni soka. Ameanza kulipwa mishahara tangu enzi akiwa mchezaji kabla ya kuhamia kwenye ukocha, ambako amepata bahati ya kuvuna mkwanja mrefu zaidi. Wakati pato lake likiripotiwa kuwa ni Dola 130 milioni, Simeone anapiga pesa nyingi sana kutokana na mshahara wake anaolipwa huko Wanda Metropolitano na kwa mwaka inaelezwa, analipwa Dola 50 milioni.
Kinachosemwa ni Simeone ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa wote wanaozinoa timu za ligi za Ulaya, akiwaburuza wote kuanzia Pep Guardiola, Jose Mourinho na makocha wengine wanaotamba kwenye ligi kubwa za Ulaya. Bado haijafahamika wazi kama Simeone ana dili zozote za kibiashara zinazomwingizia pesa za ziada, lakini kwa sasa mshahara wake ndiyo unaomfanya kuwa na mkwanja mrefu hivyo unaomfanya aishi maisha anayotaka.

Familia na makazi
Mwamba, Diego Simeone anaripotiwa kuwa na makazi yake huko Botafoc. Jumba lake hilo linaripotiwa kuwa na thamani ya Euro 2.7 milioni. Euro 2.7 milioni ni sawa na Sh7.1 bilioni. Unaweza kuvuta tu hisia, jumba la Sh7 bilioni linakuwaje. Hilo linadhihirisha wazi kocha huyo haishi kinyonge.
Kwenye jumba hilo, Simeone anaishi na mkewe, mrembo matata kabisa, Carla Pereyra, ambaye amepata naye watoto wawili wa kike, Francesca na Valentina. Wawili hao, Simeone na mrembo Carla walifunga ndoa kwa siri, Juni 2019.
Lakini, kabla ya hapo, Simeone alikuwa na mke mwingine, ambaye mke wake huyo wa kwanza, alipata naye watoto watatu wa kiume, Giovanni, Gianluca na Giuliano.

Kinachovutia watoto wake wote hao wa kiume Simeone ni wanasoka wa kulipwa, wakicheza kwenye klabu za Napoli, Rayo Majadahonda na Atletico mtawalia.
Pesa ipo, lakini haimfanyi Simeone kuishi kwa mbwembwe nyingi na hata usafiri wake anamiliki wa kawaida tu, ana magari aina ya Range Rover Sport na Hyundai, ambayo ni ya kisasa zaidi. Hata hivyo, gari hilo la Hyundai anamiliki kwa sababu ni wadhamini wake.