Duh! Mastaa kumi waomba sub

Muktasari:
- Kanuni za Kombe la Dunia la Klabu, timu zinaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano kwenye muda wa kawaida na mchezaji wa sita endapo kama mechi hiyo itaingia dakika za ziada.
MIAMI, MAREKANI: KOCHA wa Juventus, Igor Tudor amefichua kwamba wachezaji 10 walimwomba kutoka uwanjani katika mechi yao ya kipigo kutoka kwa Real Madrid kwenye kipute cha hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
Mechi hiyo ilipigwa Jumanne iliyopita huko Miami, ambapo ilichezwa kwenye hali ya hewa ya joto sana.
Kanuni za Kombe la Dunia la Klabu, timu zinaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano kwenye muda wa kawaida na mchezaji wa sita endapo kama mechi hiyo itaingia dakika za ziada.
Kocha Tudor alifanya mabadiliko ya wachezaji watano katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Juventus kukumbana na kichapo cha bao 1-0.
Baada ya mechi kocha huyo alisema: "Kuna kipindi, wachezaji 10 waliniomba kutoka, walichoshwa na hali ilivyo. Kulikuwa na ushindani mkubwa kwenye hii mechi, wachezaji walipoteza sana nguvu.
"Kisha kuna hili joto, ambalo bila shaka litakupiga, na tatu kuna hii hali ya kucheza kwenye unyevu."
Bao la kichwa la Gonzalo Garcia kwenye dakika 54 lilitosha kuleta tofauti katika mchezo huo na kuipa ushindi Real Madrid kufuatia krosi maridhawa ya Trent Alexander-Arnold.
Asisti hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Trent tangu alipojiunga na Madrid akitokea Liverpool, Mei.
Hali ya hewa imekuwa tatizo kubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu, ambapo kocha wa Chelsea, Enzo Maresca aliwahi kusema hata mazoezi yamekuwa shida kwa wachezaji kutokana na joto na mvua, ambapo imeshuhudiwa pia mechi kadhaa zikisimamishwa.