Duh! Martinez kukaa nje siku kibao

Muktasari:
- Martinez aliumia wakati alipokuwa akijaribu kunyang'anya mpira kutoka kwa Ismaila Sarr na ndipo hapo goti lake la mguu wa kushoto lilipojikunja vibaya.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imepata pigo la kumkosa beki wa kati, Lisandro Martinez kwa muda mrefu baada ya kuripotiwa kupata maumivu kwenye msuli mkubwa wa goti na kushindwa kumaliza mechi Jumapili iliyopita.
Beki huyo Muargentina mwenye umri wa miaka 27 alitolewa uwanjani kwenye machela akimwaga machozi baada ya kuumia kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace kufuatia kupata maumivu makali ya goti.
Martinez aliumia wakati alipokuwa akijaribu kunyang'anya mpira kutoka kwa Ismaila Sarr na ndipo hapo goti lake la mguu wa kushoto lilipojikunja vibaya.
Alipoanguka tu, Martinez alionyesha ishara kwa makocha wake anaomba kutoka. Hilo lilimfanya kumwaga machozi wakati alipokuwa anatolewa uwanjani.
Alipozungumza baada ya mechi, Kocha wa Man United, Ruben Amorim alikiri majeraha aliyopata Martinez ni makubwa.
Sasa taarifa za kutoka Argentina zinadai Martinez atakosa msimu wote uliobaki kutokana na majeraha hayo kwenye msuli mkubwa wa goti.
Vipimo vilivyofanywa juzi Jumatatu vilithibitisha Martinez kupata tatizo kwenye msuli wa goti lake la kushoto na sasa atalazimika kufanyiwa upasuaji, ambao unaweza kumfanya awe nje ya uwanja kwa muda unaweza kufika miezi minane.
"Si tu mchezaji mahiri bali pia ni mtu mwenye ushawishi mkubwa kwenye vyumba vya kubadilishia," alisema Amorim.
"Unapokuwa mchezaji unaona kabisa kwamba hiki kitu ni siriazi. Tupo hapa kumpa sapoti katika kipindi hiki kigumu kwake."
Martinez amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara tangu alipojiunga na Man United, Julai 2022.
Alikosa mwisho wa msimu wake wa kwanza baada ya kuvunjika mfupa wa uvugu wa mguu, lakini pia alipata maumivu ya kigimbi na goti msimu wa 2023-24.